Habari
Katibu Mkuu Kiongozi akutana na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Mjini Dodoma, 14 Septemba, 2017
Leo tarehe 14 Septemba, 2017, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mha. John W.H. Kijazi amefanya Mkutano na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaohudhuria mafunzo ya siku tano (5) yanayoendeshwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa ushirikiano na Taasisi ya Uongozi, katika Ukumbi wa Hazina Square, mjini Dodoma.
Mafunzo hayo ya Uongozi yaliyoanza tangu Jumatatu
tarehe 11 Septemba, 2017 na ambayo yanatarajiwa kuhimitimishwa siku ya Ijumaa,
tarehe 15 Septemba, 2017, yanahusisha Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa
Serikali za Mitaa wapatao 84 kutoka katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya,
Njombe, Shinyanga, Iringa, Ruvuma, Songwe na Rukwa. Mafunzo
kama hayo yalitolewa pia katika awamu zilizotangulia kwa Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi wa Serikali za Mitaa kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro,
Tabora, Kigoma, Katavi, Mwanza, Mara, Geita, Simiyu, Manyara na Kagera.
Akimkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi kuzungumza na
washiriki wa mafunzo hayo, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI,
anayesimamia Afya, Dkt. Zainab Chaula alieleza umuhimu wa mafunzo hayo ya aina
yake, yanayotolewa kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara. Alibainisha kuwa lengo kuu la mafunzo
hayo ni kuwaongezea uelewa wa masuala mbalimbali ya kiutawala, kiutumishi na
mengineyo ambayo yanahusu utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za kila siku.
Akiongea na washiriki wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu
Kiongozi aliwahimiza washiriki wa mafunzo hayo wasome, kuzielewa na
kuzizingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayohusika na masuala ya
Kiutawala na Kiutumishi ili kupata uelewa mzuri utakaowawezesha kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Sheria na Kanuni hizo ni pamoja na zile za
Mamlaka za Serikali za Mitaa; Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake; Sheria
ya Fedha za Umma na Kanuni zake; Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake; na nyinginezo.
Katibu Mkuu Kiongozi pia aliwasihi wawe karibu na
wananchi, wawasikilize na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili, kwa
kutambua kuwa lengo kuu la Serikali katika ngazi yoyote ni ustawi wa wananchi
na kwamba Serikali inawajibika kwa wananchi wake.
Akiongelea umuhimu wa udhibiti wa mapato ya Serikali
za Mitaa na matumizi ya fedha za umma, Katibu Mkuu Kiongozi aliwaagiza
washiriki wa mafunzo hayo na Uongozi wa TAMISEMI kufanyia kazi mapungufu
yaliyobainishwa katika Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali,
ikiwemo ya mwaka wa fedha 2015/ 2016.
Katibu Mkuu Kiongozi alizungumzia pia masuala
yanayogusa sekta mbalimbali zikiwemo za Maji, Nishati na Madini, Ardhi, Ujenzi
na Viwanda na Biashara, ambapo alitoa maelekezo mahsusi kwa washiriki wa
mafunzo hayo na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ujumla.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo walimshukuru Katibu Mkuu Kiongozi wa kutenga muda wake kukutana nao na kwa maelekezo yake ya kina ambayo wameahidi kuyazingatia.