Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA MILLENIUM CHALLENGE CORPORATION (MCC), 12-11-2014.


Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 12-11-2014 amekutana na Ujumbe kutoka Taasisi ya Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Corporation) ofisini kwake, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

MCC ni taasisi iliyoanzishwa na Serikali ya Marekani mwaka 2004, ili kuratibu misaada ya kiuchumi inayotolewa na nchi hiyo kwa mataifa yanayoendelea kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika kufikia Malengo ya Milenia. Tanzania ni nchi mojawapo inayonufaika na misaada hiyo ya kiuchumi kupitia mchakato wa kiushindani miongoni mwa mataifa ambayo yameonyesha matokeo chanya katika Utawala Bora, Uwezeshaji wa Wananchi na Ukuaji wa Uchumi Huru.

 

Katika mkutano huo,wajumbe kutoka taasisi ya MCC walionyesha kuridhishwa kwao na maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania katika utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na taasisi hiyo, katika kufanikisha kufikia malengo ya milenia. Miradi ambayo inatekelezwa kwa pamoja kati ya taasisi hiyo na Serikali ya Tanzania ni; Afya ya mama na mtoto, Elimu, Nishati na Upatikanaji wa maji safi na salama.

 

Ujumbe wa MCC uliongozwa na Makamu wa Rais wa taasisi hiyo, Bw. Kamran Khan. Kwa upande wa Serikali, alikuwepo pia Naibu Katibu Mkuu Ikulu, Bibi Susan Mlawi na Watendaji Waandamizi kutoka Ofisi ya Rais Ikulu.