Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi akutana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Hifadhi ya Wakimbizi Duniani Bi. Joyce Mends-Cole - 22 Februari, 2016.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 22 Februari, 2016 amekutana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Hifadhi ya Wakimbizi Duniani (UNHCR), Bi. Joyce Mends-Cole ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam.

Bi Mends-Cole alikutana na Balozi Sefue kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.

Katika mazungumzo yao, Bi Mends-Cole ameishukuru Serikali ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla kwa ushirikiano mzuri aliopewa katika kutekeleza majukumu yake yaliyohusika na masuala ya wakimbizi sehemu mbalimbali nchini Tanzania. Aidha ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa uamuzi wake wa miaka mingi na hatua inayoendelea kuchukua kuhifadhi wakimbizi toka nchi jirani na hata kufikia hatua ya kuwapa baadhi ya wakimbizi hao uraia.

Kwa upande wake, Balozi Sefue alimpongeza Bi Joyce Mends-Cole kwa mafanikio aliyopata wakati wa kutekeleza majukumu yake hapa nchini na kueleza matarajio ya Serikali ya Tanzania ya UNHCR na wadau wengine wa kimataifa kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wakimbizi na madhara mbalimbali yanayotokana na uhifadhi wa wakimbizi.

Mwisho alimtakia Bi Mends-Cole kila la kheri na maisha marefu ndani na nje ya utumishi wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.