Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI AKUTANA NA MWAKILISHI MKAZI MPYA WA BENKI YA DUNIA TANZANIA, BI. BELLA BIRD - DAR ES SALAAM, 26 AGOSTI, 2015
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 26 Agosti, 2015 amekutana na kufanya mazungumzo ofisini kwake na Mwakilishi Mkazi mpya wa Benki ya Dunia nchini, Bi. Bella Bird.
Mwakilishi Mkazi huyo aliambatana na Maafisa wengine wa Benki hiyo, Bwana Yutaka Yoshimo na Andre Bald.
Pamoja na kujitambulisha, Mwakilishi huyo alitumia fursa hiyo kuelezea masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Benki hiyo na Tanzania na namna Benki hiyo inavyoendelea kuchangia ukuaji wa uchumi na huduma za jamii kwa watanzania.
Baadhi ya maeneo yaliyozungumziwa ni pamoja na miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo ambayo ni Mradi wa Mabasi yaendayo kasi (DART), Miradi inayolenga kutekeleza Sera ya Kutambua wenye mahitaji maalum, Serikali Mtandao, n.k.
Benki ya Dunia inatarajia kuendelea kuchangia maendeleo nchini kwa kuhuisha Mkakati wa Nchi wa Ushirikiano.
Bi. Bird ambaye ni raia wa Australia na Uingereza amechukua nafasi ya Mwakilishi Mkazi aliyemaliza muda wake mwaka huu, Bwana Philip Dongier.