Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AKUTANA NA MKURUGENZI WA KITUO CHA RASILIMALI CHA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA, BI. SHEILA KHAMA, DAR ES SALAAM. 06 AGOSTI, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 6 Agosti, 2015 amekutana na Mkurugenzi wa Kituo cha Rasilimali cha Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Natural Resources Center), Bi. Sheila Khama.

Bi. Khama aliambatana na Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo, Dkt. Tonia Kandiero pamoja na mtaalam kutoka Kituo hicho, Bw. Thomas Viot.

Mazungumzo kati ya ujumbe huo na Katibu Mkuu Kiongozi yalihusu mpango wa benki hiyo wa kufadhili programu ya kujenga uwezo wa wataalam mbalimbali wa kitanzania wanaohusika na sekta ya gesi, mafuta na rasilimali nyinginezo, kama vile madini.

Benki hiyo imedhamiria kutekeleza azma hiyo kupitia Wizara husika na imepanga kuitumia Taasisi ya UONGOZI katika kufanikisha programu hiyo ambayo inayotarajiwa kuanza miezi michache ijayo.

Balozi Sefue ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo mkubwa kwani kwa kujengewa uwezo wataalam wa Tanzania watamudu vema kusimamia sekta hii muhimu kwa manufaa makubwa kwa Taifa.