Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AKUTANA NA KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA BIASHARA WA NCHI YA IRELAND - 08/09/2014


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue, amekutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara wa nchi ya Ireland Bw.  Niall Burgess kwa mazungumzo mafupi, leo tarehe 8/9/2014 ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam.

Katika mkutano huo Bw. Burgess aliambatana na ujumbe wa maofisa mbalimbali wa nchi hiyo kutoka ofisi za ubalozi wa nchi hiyo hapa Tanzania akiwemo Balozi wa Ireland nchini Bi. Fionnuala Gilsenan.

Katika Mazungumzo hayo, Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili kutokana na ushirikiano wake wa kihistoria. Balozi Sefue alibainisha kuwa serikali iko katika mkakati wa kuboresha Sekta ya kilimo ili kuwaendeleza wakulima kutoka katika kilimo cha uzalishaji wa kujikimu na kuwa uzalishaji mkubwa wa kibiashara, hivyo basi kunahitajika ushirikiano mkubwa na nchi wahisani ikiwamo Ireland katika kusaidia katika bajeti hasa katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wake Bw. Burgess aliunga mkono mpango huo wa serikali ya Tanzania na kuahidi kuwa nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwamo Kilimo, Elimu na TEHAMA pamoja na kusaidia kuchangia katika Bajeti ya maendeleo.

Mwishoni wa mazungumzo hayo Katibu Mkuu huyo pamoja na ujumbe wake waliahidi kuendelea kufanyia kazi mambo mbalimbali waliyoyazungumzia ili kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na maofisa mbalimbali wa serikali ya Tanzania kutoka Ofisi ya Rais Ikulu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Akiwaaga wageni wake hao, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwashukuru kwa ujio wao huo na kuwaomba wasisite kuja kufanya majadiliano  katika mambo mbalimbali ili kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.