Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AKAMILISHA ZIARA YAKE YA KIKAZI MKOANI MANYARA - 17 SEPTEMBA 2014.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani Manyara tarehe 17 Septemba, 2014 kwa kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.

Ziara ya Katibu Mkuu Kiongozi ilianzia katika Ofisi ya Sekretarieti ya Mkoa wa Manyara ambapo Katibu Mkuu Kiongozi alisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa Mhandisi Omari Chambo. Baadaye, Katibu Mkuu Kiongozi alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Elaston J. Mbwilo ambako alipokea taarifa fupi ya mkoa kuhusu hali ya maendeleo, ulinzi na usalama.

Baada ya hapo, Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kukutana na Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Manyara na baadhi ya Watumishi wa Taasisi za Umma zilizopo Mkoani humo ambako alisisitiza kuwa Watumishi wote wa Umma wanafanya kazi kwa niaba ya Rais, hivyo katika kutekeleza jukumu hilo la Rais ni sharti wazingatie Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa kwa misingi hiyo.

Katika kusisitiza umuhimu huo, Katibu Mkuu Kiongozi alisema "Watumishi wa Umma ni lazima kuwa waadilifu, waaminifu, weledi, wanyenyekevu, wazingatiaji wa nidhamu, wastahimilivu na wepesi wa kuzingatia staha ili wananchi waweze kutoa mrejesho wa huduma bora waliyopewa". Mtumishi wa Umma sharti ajiulize baada ya mwananchi kuhudumiwa anaondoka na sura ipi kuhusu Utumishi wa Umma", aliagiza.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, alisisitiza pia kuwa katika dunia ya sasa ni ya TEHAMA na haikwepeki. Hata hivyo, alibainisha kuwa licha ya matumizi hayo ya TEHAMA kuwa ya manufaa, Watumishi wa Umma wazingatie kuwa kumbukumbu ya masuala ya Serikali yanapaswa kubakia kuwa siri kubwa. Hivyo, Serikali inaendelea kuweka mifumo ya kuhakikisha mifumo hiyo inakuwepo na akawajulisha Watumishi kuwa kutakuwa na anuani rasmi za mawasiliano rasmi ndani ya Serikali mtandao kupitia Wakala ya Serikali Mtandao.

Mwisho, Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza kuwa uadilifu ndani ya Utumishi wa Umma ni msingi mkuu wa Utumishi wa Umma na kwamba unapaswa kuenziwa na kuheshimiwa.

Baada ya kumaliza kikao chake, Balozi Sefue pamoja na ujumbe wake walienda kuona mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, na vilevile walipata fursa ya kuona nyumba ya makazi ya kiongozi (state lodge) iliyojengwa kwa gharama za Serikali.

Baada ya mapumziko mafupi, Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na ujumbe wake walirejea mkoani Arusha ambako wanatarajia kuwa na ziara ya kikazi ya siku moja tarehe 18/9/2014 na kumalizia ziara yake hii katika mkoa wa Kilimanjaro tarehe 19/9/2014.