Habari
Katibu Mkuu kiongozi akagua maandalizi ya sherehe ya uzinduzi wa jengo jipya la ofisi ya Rais, Ikulu Chamwino – 10 Mei, 2023
Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses M. Kusiluka leo tarehe 10 Mei, 2023 amefanya ukaguzi wa maandalizi ya sherehe za uzinduzi wa jengo jipya la ofisi ya Rais, Ikulu lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Ujenzi wa jengo jipya la Ikulu ya Chamwino ulioanza mwaka 2020 umekamilika na linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Mei, 2023.
Akizungumza na Kamati ya Maandalizi ya sherehe hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza na kuelekeza kwamba, kazi zilizosalia katika maandalizi hayo, zikamilishwe mapema kama ilivyopangwa.
Sherehe hiyo ya kihistoria inatarajiwa kuhudhuriwa na takribani watu 2,500.