Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi akabidhi ndege aina ya Fokker 50 kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) - 01 Aprili, 2019Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John W. H. Kijazi, leo amekabidhi ndege ya Serikali aina ya Fokker 50 kwa shirika la ndege la Tanzania ATCL. Makabidhiano hayo yamefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, tarehe 01 Aprili, 2019

Katika hotuba yake fupi ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Kiongozi alikumbusha kuhusu maagizo aliyoyatoa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 11 Januari 2019, wakati wa hafla ya mapokezi na makabidhiano ya ndege aina ya Airbus 220-300 iliyofanyika kiwanjani hapo, kuwa ndege mbili za Serikali, aina ya Fokker 50 na Fokker 28 ambazo zinatumika kwa safari za Viongozi Wakuu wa Serikali nazo ziwekwe nembo (zipakwe rangi na kuchora picha ya Twiga) ya Air Tanzania na zikodishwe kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili ziweze kutumika kubeba abiria kwa sababu si kila wakati zinatumika kwa ajili ya shughuli za Serikali. Hatua ambayo ni muhimu katika juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba usafiri wa anga nchini unaimarika na wananchi wanawezeshwa kufanya shughuli zao za maendeleo na za kijamii kwa urahisi na kwa haraka zaidi.

“Sote tunafahamu kwamba hadi sasa Serikali imeshanunua ndege mpya sita (6) ambazo ni: Bombardier Q400-8 (3), Boeing 787-8 Dreamliner (1), na Airbus 220-300 (2). Ndege zote sita zimekodishwa kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na zinafanya kazi. Ndege nyingine mpya mbili zaidi, ambazo ni Boeing 787-8 Dreamliner na Bombardier Q400-8), zimeagizwa na zinatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka huu”. Alisisitiza Katibu Mkuu Kiongozi

Katika Makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Kiongozi alitiliana saini mkataba wa makabidhiano baina ya Serikali na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambapo Katibu Mkuu (Uchukuzi) Dkt. Leonard Chamuriho ndiye aliyesaini mkataba huo. Baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali waliohudhuria hafla hiyo ni Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Ikulu, Bwana Benjamin Ndimila, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Ndege la ATCL Mhandisi Emmanuel Korosso pamoja na watumishi wa Wakala wa Ndege za Serikali na ATCL.

NB: Hotuba kamili ya Makabidhiano inapatikana katika tovuti rasmi ya Katibu Mkuu Kiongozi www.chiefsecretary.go.tz