Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI KANDA YA ZIWA, 6 AGOSTI, 2014


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, tarehe 6 Agosti, 2014 amehitimisha ziara yake ya kikazi ya Mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza kwa kufanya mazungumzo na Uongozi na Watumishi wa Seketarieti ya Mkoa wa Mwanza, Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela, Taasisi na Wakala za Serikali zilizopo Mkoani Mwanza. Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Mwanza.

 Ziara hiyo ya kikazi ilianzia Mkoani Mara tarehe 4 Agosti, 2014 na katika Mkoa mpya wa Simiyu siku iliyofuata tarehe 5 Agosti, 2014.

Akihitimisha ziara hiyo, Balozi Sefue alirejea kuwakumbusha Viongozi na Watumishi wa Umma kuhusu umuhimu wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa. Aidha, alisisitiza uadilifu, uaminifu na weledi katika Utumishi wa Umma.

Alisema kumejitokeza wimbi la ukiukwaji mkubwa wa maadili, wizi, udanganyifu, kutojali na kutotii sheria, uzembe na kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika. "Hali hii ikiachiwa kuota mizizi italeta athari kubwa katika Utumishi wa Umma, kwa nchi na Taifa kwa ujumla, alisisitiza. Hivyo, hapana budi kwa kila mmoja wetu kwa nafasi yake kukemea na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kinidhamu wahusika pindi wanapotenda kosa na sio kwa kuwahamisha".

Akifafanua kuhusu uamuzi wa Serikali wa kukasimu mamlaka ya kuajiri kwa kada 22 kwa Serikali za Mitaa, Balozi Sefue alitoa angalizo kuwa hatua hiyo haikumaanisha kubadili Sera, Sheria na taratibu za ajira. Hivyo, katika mchakato wa ajira, Halmashauri zinapaswa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za ajira zilizopo na akazitaka halmashauri zitumie utaalamu na ushauri wa Sekretarieti ya Ajira.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi alipata pia fursa ya kusalimiana na Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Evarist Ndikilo ambaye alitoa taarifa fupi ya Mkoa kabla ya kumpitisha kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi mpya za Mkoa.