Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AHIMIZA MASUALA MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA KIPINDI CHA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU UTAKAOFANYIKA NCHINI MWEZI OKTOBA, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 22 Julai, 2015 amefungua Mkutano wa Mwaka wa Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa na kuhimiza masuala muhimu ya kuzingatia wakati nchi ikielekea katika Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika katika kituo cha mikutano cha Mtakatifu Gasper kilichopo mjini Dodoma kuanzia tarehe 22 - 23 Julai, 2015.

Sisi Watendaji Wakuu tunayo dhamana kubw katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu. Kila mmoja wenu azijue sheria, kanuni na taratibu zinazohusiana na Uchaguzi Mkuu, pamoja na kujua namna ya kuendesha shughuli za Serikali katika kipindi hiki, alisema.

Aidha Balozi Sefue alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Watendaji Wakuu hao kusimamia kwa dhati nidhamu ya watumishi wanaowasimamia na kuwataka kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wakosaji bila woga wala upendeleo.

Katika ufunguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Galawa aliwakaribisha wajumbe wa mkutano na kuwasihi wawahimize watumishi wa Umma kuwafuata wananchi waliko na kuwahudumia badala ya kukaa ofisini hali ambayo inalalamikiwa sana.