Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AHIMIZA MABALOZI KUSIMAMIA KWA DHATI MISINGI YA UTAWALA BORA NA RASILIMALI ZA TAIFA, HOTELI YA RAMADA, DAR ES SALAAM, 26 MEI, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo, tarehe 26 Mei, 2015 katika Hoteli ya Ramada iliyopo Kunduchi jijini Dar es Salaam, amewasilisha mada kwenye Mkutano wa Nne wa Mabalozi wa Tanzania nchi za nje inayohusu Utawala Bora na Usimamizi wa Rasilimali za Taifa, ambapo amewahimiza kusimamia kwa dhati misingi ya Utawala Bora na Rasilimali za Taifa.

Balozi Sefue alifafanua kuwa ........ Utawala bora ni ule unaozingatia na kujali matakwa na maslahi ya wengi na  unaosisitiza kuheshimu sheria, uwajibikaji wa viongozi, kupiga vita rushwa na kuboresha maisha ya raia. Ni utawala unaozingatia kwa dhati matumizi sahihi ya nyenzo na rasilimali za taifa, uadilifu, misingi na taratibu zinazokubalika ili kukidhi maslahi ya taifa. Aidha, mfumo wa utawala bora unahusisha matumizi sahihi ya madaraka. Vile vile, utawala bora unasisitiza ufanisi katika utendaji kazi; utoaji huduma ulio bora; uongozi ulio adilifu na wenye hekima; uwazi na uwajibikaji katika shughuli za umma na uangalifu na uadilifu katika matumizi ya nyenzo za Serikali.

Mkutano huo uliobeba kauli mbiu Diplomasia ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa 2025 ulifunguliwa na Mhe. Dk. Jakaya M. Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na unatarajiwa kufungwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

NB: Mada ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika Tovuti hii.