Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI, AFUNGUA SEMINA YA KUJENGA UELEWA WA PAMOJA KUHUSU UENDESHAJI WA MASOKO YA BIDHAA, DAR ES SALAAM 29 JULAI, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe  29 Julai, 2015 amefungua Warsha ya siku mbili inayowakutanisha Wataalam na Waandaaji wa sera kuhusu uendeshaji wa masoko ya bidhaa nchini.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA) inafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu na itahitimishwa tarehe 30 Julai, 2015. Washiriki wa Warsha hiyo ni Watendaji Waandamizi kutoka Serikalini na Sekta binafsi.

Balozi Sefue ameelezea umuhimu wa kuwa na masoko ya bidhaa nchini kwani yanatoa fursa ya washiriki kuweza kuuza au kubadilishana bidhaa kwa njia ya uwazi unaotoa mwanya wa kila upande kunufaika (win-win outcome) na pia kuwepo kwa uwezekano wa kuongeza mnyororo wa thamani ya bidhaa.

Masoko ya bidhaa ya aina hii yanakusudiwa kuanzishwa nchini kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Masoko ya Bidhaa ya Mwaka 2015 na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao chake cha Ishirini (20) kilichomalizika mwezi huu.

 

NB: Soma hotuba kamili ya Katibu Mkuu Kiongozi kupitia tovuti hii.