Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AFUNGUA PROGRAMU YA MAFUNZO KWA TIMU YA SERIKALI YA MAJADILIANO YA MIKATABA YA GESI ASILIA NA MAFUTA (GOVERNMENT TEAM OF NEGOTIATORS) - PARK HYATT HOTEL 05 MEI, 2015.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 5 Mei, 2015, amefungua Programu ya Mafunzo kwa Timu ya Serikali ya Majadiliano ya Mikataba ya Gesi Asilia na Mafuta (Government Team of Negotiators) katika Hoteli ya Park Hyatt mjini Zanzibar. Mafunzo hayo ni mahsusi kwa ajili ya kuwajengea wataalam hao wa Serikali uwezo wa kujadili na kufikia makubaliano ya mikataba ya kusimamia Sekta ya Gesi Asilia na Mafuta ili iweze kuleta manufaa yanayotarajiwa nchini.

Timu hiyo inashirikisha wataalam kutoka Sekta zote muhimu zinazohusisha Sekta ya Gesi Asilia na Mafuta.

Akifungua warsha ya kwanza ya mafunzo hayo, Balozi Sefue alieleza kwamba Serikali imewapa jukumu kubwa na inaamini kuwa watajifunza, watatafiti na kushauri namna bora ya Serikali kunufaika na Sekta hii ya Gesi Asilia na Mafuta. Na akahimiza watekeleze matarajio hayo kwa ukamilifu.

Aidha, aliwashukuru wafadhili wa programu ambao ni The Bill and Melinda Gates Foundation na UNDP  kwa msaada wa kifedha utakaowezesha programu hii na akahimiza wafadhili wengine kujitokeza kwani ni programu inayokusudia kujenga uwezo wa wataalam wa kitanzania watakaosimamia Sekta hii kwa miaka mingi ijayo. Vile vile, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kukubali kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa programu hii muhimu kwa Taifa.

 

NB: Hotuba kamili ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika tovuti hii