Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AFUNGUA MKUTANO WA KWANZA WA MWAKA KUHUSU SERIKALI MTANDAO (1ST ANNUAL e-GOVERNMENT CONFERENCE) ARUSHA NA KUAGIZA MTINDO WA KUDURUFU MIFUMO YA TEHAMA UKOME, ARUSHA. 19 AGOSTI, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 19 Agosti, 2015 amefungua Mkutano wa Kwanza wa Mwaka kuhusu Serikali Mtandao unaofanyika ktika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Mkutano huu unawakutanisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi mbalimbali za Taasisi za Serikali, Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Wakala wa Serikali kwa lengo la kujadili kwa kina mtazamo na msukumo mpya wa utekelezaji wa malengo ya Serikali Mtandao.

Akifungua Mkutano huo, Balozi Sefue amebainisha wazi kuwa matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa shughuli za Serikali si jambo la hiari bali ni la lazima.

Mkutano huu ni moja ya mikakati ya kujengea na kuboresha uwezo ndani ya Serikali na taasisi zake wa kuimarisha mawasiliano miongoni mwa wadau, kubadilishana uzoefu na kuhamasisha matumizi ya TEHAMA yenye tija katika kuboresha utendaji wa taasisi za umma katika kuhudumia na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi, alisisitiza.

Aidha, Balozi Sefue aliainisha baadhi ya mambo makubwa yanayokwamisha ufanisi wa mwelekeo katika Serikali Mtandao ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa mfumo mmoja ulio chini ya chombo au mamlaka moja katika kutambua na kusajili watu na kutokuwepo kwa uwiano wa kutosha kati ya taratibu za utendaji kazi Serikalini (Government Business Process) na teknolojia inayotumika.

Alieleza matokeo yake yanakuwa ni pamoja na Serikali haipati thamani halisi ya fedha zinazotolewa kwenye miradi ya TEHAMA, Taasisi za Serikali zinakuwa na mifumo ambayo haiongei na haiwezi kuwasiliana na kubadilishana taarifa (ndani ya taasisi, na kati ya taasisi na taasisi), Urudufu wa mifumo miongoni mwa taasisi za Serikali yenye viwango tofauti, Msukumo na utegemezi wa wakandarasi kwa kiasi kikubwa katika kushauri, kubuni, kusimamia na kuhifadhi mifumo ya TEHAMA ya Serikali, Uhusiano na uratibu hafifu wa shughuli za TEHAMA ndani na kati ya Taasisi za Serikali, Ukosefu wa njia za kutosha za kutoa huduma za Serikali Mtandao (service delivery channels), Idadi ndogo ya huduma na taarifa za Serikali zinazotolewa kupitia TEHAMA, Kuongezeka kwa matishio ya usalama wa taarifa katika mifumo ya TEHAMA.

 

Balozi Sefue alibainisha kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali imeweka msukumo mpya katika kutekeleza Serikali Mtandao kwa kusisitiza ushirikiano na matumizi ya pamoja ya rasilimali TEHAMA miongoni mwa taasisi za umma, kujenga uwezo wa taasisi za umma na watumishi wake katika matumizi ya TEHAMA, kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, kuimarisha uratibu wa shughuli za TEHAMA na usalama wa taarifa za Serikali.

 

NB:Hotuba kamili ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika tovuti hii