Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI AFUNGUA MKUTA NO WA 29 WA WATAFITI ULIOANDALIWA NA TAASISI YA UTAFITI WA MAGONJWA YA BINADAMU (NIMR) NA KUSISITIZA MATUMIZI YA MATOKEO YA UTAFITI WAKATI WA KUTENGENEZA SERA NA UTEKELEZAJI WAKE, DAR ES SALAAM, TAREHE 13 OKTOBA, 2015.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 13 Oktoba, 2015 amefungua Mkutano wa 29 wa Watafiti ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa na Binadamu (NIMR) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na kupokea Tuzo maalum iliyotolewa kwa Rais, Balozi Sefue aliipongeza NIMR na Taasisi nyingine za utafiti wa magonjwa ya binadamu kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanya tafiti na kutumia matokeo ya tafiti hizo kupambana na changamoto za kiafya zinazoikabili jamii yetu.
Balozi Sefue alieleza nia thabiti iliyoonyeshwa na Serikali ya Awamu ya Nne katika kuongeza bajeti, rasilimali na mafunzo kwa watafiti wa Tanzania. Alihimiza Serikali kuendeleza nia hiyo ya dhati hasa kipindi hiki ambaccho jamii yetu inakabiliana na magonjwa mbalimbali ya kuambukizwa (communicable diseases) na yasiyoambukizwa (non communicable diseases).
Aidha, alihimiza Watafiti wa Tanzania kuongeza nguvu zaidi za utafiti na kutafuta ufumbuzi wa kitabibu kwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile Saratani, Shinikizo la damu na Kisukari, ambayo kwa mujibu wa takwimu, yameongezeka kwa kasi katika jamii yetu.
Katika Mkutano huo, watafiti watano (5) walitunukiwa Tuzo maalum ikiwa ni kutambua mchango mkubwa uliotokana na tafiti zao.
Mkutano huo wa siku tatu unahudhuriwa na watafiti wa ndani na wa nje wapatao 250.
NB: Soma Hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi katika Tovuti hii