Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AFUNGUA MAADHIMISHO YA KUMI NA TATU (13) YA SIKU YA WAHANDISI NCHINI NA KUSISITIZA WAHANDISI KUZINGATIA NA KUHESHIMU VIAPO VYA KAZI ZAO, DAR ES SALAAM - 3 SEPTEMBA, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 3 Septemba, 2015 amefungua Maadhimisho ya 13 ya mwaka 2015 ya Siku ya Wahandisi nchini yaliyoambatana na Kongamano la siku mbili na maonyesho mbalimbali katika Ukumbi wa Mlimani City. jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Kiongozi alialikwa kufungua maadhimisho hayo na pia kutoa Hotuba ya Msingi (Keynote Address) kuhusu Miaka 15 ya Utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Nafasi ya Wahandisi.

Akizungumza baada ya kushuhudia Wahandisi wapya wakila Kiapo cha Uadilifu, Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza kuwa ni muhimu na ni wajibu Wahandisi hao watekeleze viapo hivyo kwa ukamilifu, uadilifu na uaminifu kwa kadiri ya matakwa ya viapo. Aidha, aliwahimiza kuendelea kufanya kazi zao kwa uhodari na kwa kutumia weledi, bidii na maarifa ili kuweza kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Umuhimu wa wahandisi kwa maendeleo ya taifa letu umeelezwa wakati wote na uko dhahiri. Ni ukweli usiopingika kuwa bila ya wahandisi hakuna maendeleo, alibainisha.

Vilevile, Katibu Mkuu Kiongozi alisifu na kuhimiza ushirikiano miongoni mwa wahandisi wa nchi za Afrika kwani mazingira na changamoto wanazokumbana nazo yanafanana hivyo kurahisisha ufumbuzi wa pamoja wa changamoto hizo.

Pamoja na washiriki wa ndani wanaofikia takriban 2,000, kongamano hili la siku mbili linahudhuriwa na wahandisi waalikwa kutoka nchi za Kenya, Malawi, Afrika Kusini na Nigeria.

NB: Soma hotuba kamili na Hotuba ya Msingi (keynote address) kupitia tovuti hii.