Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi afungua Kikao Maalum cha Kazi kwa Watendaji wa Bodi za Kitaaluma na Mamlaka za Uthibiti na Ithibati ya Elimu na Mafunzo.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 12 Novemba, 2015 amefungua Kikao Maalum cha Kazi kwa Watendaji wa Bodi za Kitaaluma na Mamlaka za Uthibiti na Ithibati ya Elimu na Mafunzo, katika Hoteli ya Whitesands, jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, Katibu Mkuu Kiongozi alieleza azma ya Serikali kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa na taasisi za elimu na mafunzo hapa nchini inakidhi viwango vya ubora kitaifa na kimataifa. Ili kutimiza azma hiyo, Balozi Sefue alihimiza Bodi za kitaaluma na Mamlaka za Uthibiti na Ithibati kutekeleza ipasavyo wajibu wao. Alielekeza vyombo vya kitaalamu vibaki kwenye eneo lake la kudhibiti na kuendeleza wanaoingia katika eneo la utaalam wanaousimamia na vya Uthibiti na Ithibati wa ubora wa elimu na mafunzo vibaki pia kwenye eneo lao pasipo kuingiliana lakini vishirikiane.

Balozi Sefue aliwahasa Watendaji wa Bodi na Mamlaka waliohudhuria kikao hicho maalum cha kazi, kujadili kwa uwazi na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kisheria na kiutendaji zinazojitokeza miongoni na baina ya Mamlaka na Bodi zao.

Miongoni mwa changamoto zitakazotafutiwa ufumbuzi ni pamoja na migongano iliyojitokeza hivi karibuni  kuhusu nani mwenye mamlaka juu ya baadhi ya masuala yanayohusu utoaji wa elimu na mafunzo hapa nchini.

Kikao hicho cha siku mbili kinaendeshwa na Taasisi ya Uongozi na kuhudhuriwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha, Elimu, Mifugo na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Pia kinahudhuriwa na Watendaji Wakuu wa Bodi na Mamlaka za Uthibiti na Ithibati wa Elimu na Mafunzo ikiwemo VETA, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

 

NB: Soma hotuba ya kamili ndani ya Tovuti hii.