Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AFUNGA MAFUNZO ELEKEZI KWA MAKAMISHNA WA TUME YA UTUMISHI WA UMMA, HOTELI YA OCEANIC BAY, BAGAMOYO, 30 APRILI, 2015.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 30 Aprili, 2015 amefunga Mafunzo Elekezi yaliyoandaliwa na Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya Makamishna wapya wa Tume hiyo katika Hoteli ya Oceanic Bay mjini Bagamoyo.

Mafunzo hayo yalianza Jumatatu tarehe 27 Aprili, 2015 ambapo yalifunguliwa rasmi tarehe 28 Aprili, 2015 na Mhe. Celina Kombani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Mafunzo yalilenga pamoja na mambo mengine kutoa fursa kwa Makamishna wapya kufahamiana na kuwajengea uelewa wa pamoja wa majukumu yao mapya kwenye Tume hiyo.

Katika hotuba yake ya kufunga mafunzo hayo, Katibu Mkuu Kiongozi ameelezea matarajio yake kuwa baada ya kuyatambua majukumu yao vema kupitia mafunzo hayo, Makamishna hao watatekeleza majukumu hayo kwa ukamilifu na kwa ufanisi na bila mikwaruzano na migongano.

Aidha, amewataka kushughulikia kwa mpango wa dharura rufaa ambazo zitakuwa zimewasilishwa katika Tume katika kipindi chote ambacho Tume ilikuwa haijateuliwa na akawaahidi ushirikiano unaostahili kuwawezesha kutimiza matarajio aliyonayo Mheshimiwa Rais kwa Tume hiyo.

NB: Hotuba kamili ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika Tovuti hii.