Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AFUNGA KONGAMANO LA SIKU MOJA LILILOANDALIWA NA TUME YA UTUMISHI WA UMMA KUADHIMISHA MIAKA KUMI (10) YA UHAI WAKE TAREHE 30 OKTOBA, 2014


Tarehe 30 Oktoba, 2014 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue alishiriki katika Kongamano la siku moja lililoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Umma, mahsusi kwa ajili ya kuadhimisha miaka 10 ya kuanzishwa kwake. Kongamano hilo lilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius K. Nyerere na lilifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete .

Mawaziri mbalimbali, Makatibu Wakuu, Watendaji Waandamizi, Wakurugenzi Watendaji na Maafis Waandamizi wa Serikali na Taasisi za Umma walishiriki katika Kongamano hilo, ambalo lilifana sana.

Katika hotuba yake ya kufunga Kongamano hilo, Balozi Sefue aliipongeza sana Tume ya Utumishi wa Umma kwa mafanikio makubwa iliyopata kwa kipindi cha miaka kumi (10) iliyopita na akawatakia kila la kheri katika kufikia matarajio waliyoainisha katika taarifa yao ya utekelezaji.

Aidha, Balozi Sefue alisisitiza masuala yaliyobebwa na Kaulimbiu ya Kongamano hilo, yaani “Uzalendo, Uadilifu na Uwajibikaji katika kusimamia rasilimali watu ndani yaUtumishi wa Umma kwa lengo la kukua uchumi na kupunguza umasikini”.

 “Kila mtumishi wa Umma akizingatia kwa ukamilifu dhana iliyobebwa na kauli ya Kongamano hili, tutakuwa chachu ya maendeleo ya Taifa na tutaboresha sura ya Utumishi wa Umma machoni mwa wananchi,” alisema.

Kuhusu kuimarisha usimamizi wa menejimenti ya rasilimali watu katika utumishi wa Umma, Balozi Sefue alisema Ofisi yake inafuatilia kwa karibu sana utekelezaji wa majukumu hayo na akaeleza kuwa atahitaji kupatiwa kila mara taarifa za utekelezaji wa yale yaliyoazimiwa katika kongamano hilo. Akahimiza kuwa pale patakapokuwa na vikwazo vyovyote, atapenda apatiwe taarifa mapema ili, kwa kushirikiana pamoja, vipatiwe ufumbuzi.