Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AFANYA ZIARA KATIKA KONGANI YA VIWANDA KWALA MKOANI PWANI


Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka amebainisha kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji katika ujenzi wa Kongani ya Viwanda unaoendelea katika eneo la Kwala mkoani Pwani.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Kusiluka ameyasema hayo Januari 5, 2024 akiongozana na baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakuu wa Taasisi mbalimbali katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kongani ya Viwanda ya SINO TAN inaotarajiwa kuwa na viwanda zaidi ya 200 katika eneo la Kwala Mkoani Pwani ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufanya ziara hiyo kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi huo.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan inaunga mkono jitihada zinazofanywa na wawekezaji na itahakikisha mradi huo muhimu na wenye faida nyingi hususan katika kuongeza ajira, pato la Taifa na ukuaji wa uchumi kwa ujumla unakamilika kama ilivyokusudiwa.