Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi , afanya mazungumzo na Bw. Serge Brammertz


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi, Jana, tarehe 13 Aprili, 2016, alikutana kwa mazungumzo na Bw. Serge Brammertz, Mwendesha Mashtaka wa Chombo cha Kimataifa kilichoundwa kushughulikia masalia ya zilizokuwa Mahakama za Kimataifa za Makosa ya Kimbari yaliyotekelezwa nchini Rwanda (ICTR) na iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia (ICTY) ijulikanayo kwa Kiingereza kama Mechanism for International Criminal Tribunals (MICT).

Bw. Brammertz alimtembelea Katibu Mkuu Kiongozi kwa lengo la kujitambulisha, kufuatia uteuzi wake kushika wadhifa huo kuanzia tarehe 1 Machi, 2016 hadi tarehe 30 Juni, 2018, ambapo atakuwa na Ofisi The Hague, Uholanzi na Arusha, Tanzania. Mgeni huyo aliambatana na Bw. Abubacarr Tambadou, Msaidizi Maalum wa Mwendesha Mashtaka na Bw. Kevin Hughes, Mshauri wa Sheria wa Mwendesha Mashtaka wa MICT.

Katika mazungumzo yao, Bw. Brammertz alielezea kuridhishwa na mapokezi mazuri aliyopatiwa na Serikali ya Tanzania, ambapo amepata fursa ya kukutana na Watendaji Wakuu mbalimbali akiwemo Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman. Aidha, aliahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha majukumu ya msingi ya MICT na kukuza hadhi ya Arusha ili izidi kufahamika kote ulimwenguni kama Makao Makuu ya Taasisi za Kisheria na Utoaji Haki za Kimataifa barani Afrika.

Pamoja na kutekeleza majukumu ya MICT yaliyopitishwa kwa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mgeni huyo alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika mafunzo kwa waendesha mashtaka na wanasheria ili kuiwezesha Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kufaidika zaidi na uwepo wa MICT. Wawili hao walikubaliana kulifanyia kazi wazo hilo mapema iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi kwa mara nyingine tena aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuiamini Tanzania na kuipa heshima ya kuwa mwenyeji wa MICT kwa upande wa Afrika. Aidha, aliahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano unaotakikana kwa MICT ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ikiwemo kukamilisha mashauri na rufaa zilizosalia, kuwatia nguvuni watuhumiwa (fugitives) na kuwatafutia wafungwa makazi katika nchi ya tatu. Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi aliahidi kushirikiana na MICT kufanikisha mipango mingine endelevu ya MICT yenye manufaa kwa pande zote mbili, wadau wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.