Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi aendesha mkutano wa Taasisi za Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Silaha za Maangamizi. 20/07/2023


Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka, na Katibu Mkuu Kiongozi  wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mhandisi Zena A. Said wameendesha mkutano wa Taasisi za udhibiti wa utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi za Tanzania Bara na Zanzibar. Mkutano huo  ulioandaliwa na Wizara ya Fedha na kuhudhuriwa na Makatibu Wakuu na Wakuu wa  Taasisi hizo, ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam. Ikiwa ni jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutathimini utekelezaji wa viwango vya Kimataifa vya udhibiti wa utakasishaji fedha haramu ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi. Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Emanuel Tutuba na Naibu Katibu Mkuu  wa Wizara ya Fedha Bw. Elija Mwandumbya ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

Katika mkutano huo, wataalam walisisitiza taasisi husika kutilia mkazo elimu kwa umma ili kufanikisha juhudi za serikali katika udhibiti wa utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi na kuzijengea uwezo taasisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria zinazounda taasisi hizo.

Aidha, maelekezo yalitolewa kwamba kuwepo na miongozo ya kuziwezesha taasisi za usimamizi namna nzuri na kuweza kutambua vihatarishi vya utakasishaji fedha haramu ufadhili  wa ugaidi na ufadhili wa  silaha za maangamizi.