Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AENDELEA NA ZIARA YA KIKAZI MKOANI ARUSHA, 18 SEPTEMBA, 2014


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 18 Septemba, 2014 ameendelea na ziara yake ya kikazi ya Kanda ya Kaskazini kwa kutembelea Mkoa wa Arusha. Katika ziara yake hiyo aliambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Bw. Jumanne A. Sagini na Watendaji Waandamizi kutoka TAMISEMI na Ofisi ya Rais Ikulu.

Kabla ya kupata fursa ya kuzungumza na Menejimenti na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Arusha, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na Wakala za Serikali zilizopo mkoani humo, Katibu Mkuu Kiongozi alitembelea na kuona Mfumo wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa wa kukusanya mapato katika Jiji la Arusha ambao umeliwezesha Jiji hilo kuongeza mapato kwa zaidi ya asilimia sitini na nne (64%) kwa mwaka wa fedha wa 2013/14. Kutokana na mafanikio ya mfumo huo, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa rai kuwa, Halmashauri zingine hapa nchini hazina budi kujifunza kutoka Jiji la Arusha.

Aidha, Balozi Sefue alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru ambapo alionyeshwa Mfumo wa Kielektroniki wa uchangiaji huduma za afya. Akiwa katika hospitali hiyo, aielezwa kuhusu mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na upanuzi wa hospitali hiyo ili kuipa hadhi ya Kimataifa.

Katika vikao vya Menejimenti na Watumishi, Balozi Sefue alirejea msisitizo wake kuwa Watumishi wa Umma wawahudumie wananchi kwa weledi, uadilifu, uaminifu na unyenyekevu mkubwa ili kutoa taswira nzuri ya Serikali kwa wananchi. "Kwa nafasi yenu ninyi ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais na Serikali yake katika ngazi za kila mmoja wenu", aliwaasa. Hivyo Watumishi wa Umma wanapaswa kuzingatia wajibu huo mkubwa.

Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza juu ya umuhimu wa kila mmoja kuwa sehemu ya ulinzi na usalama wa nchi badala ya kuachia vyombo vya ulinzi na usalama pekee.

Vilevile, aliwakumbusha Watumishi kutojihusisha na masuala ya Siasa kwa kuwa ni kinyume na misingi ya Utumishi wa Umma. Hali kadhalika, alisisitiza umuhimu wa kutunza vizuri kumbukumbu na nyaraka za Serikali na akaonya kuwa mtumishi yeyote atakayevujisha siri za Serikali atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Balozi Sefue alionya dhidi ya tabia inayozidi kujengeka sana miongoni mwa wananchi na hata Watumishi wa Umma ya kutojali sheria na hata kujichukulia sheria mkononi. Akasisitiza kuwa watakaojihusisha na tabia hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwisho, Katibu Mkuu Kiongozi alikemea tabia ya Watumishi wa Umma ya kuwasilisha madai yasiyo halali na hivyo kuisababishia Serikali hasara kubwa. Akaonya kuwa Watumishi pamoja na viongozi watakaobainika kujihusisha na madai ya namna hiyo, watashughulikiwa bila kujali nafasi zao.

Baada ya kumaliza vikao hivyo, Balozi Sefue pamoja na ujumbe wake walielekea Mkoani Kilimanjaro ambako atahitimisha ziara yake hiyo ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini.