Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi aelezea kuhusu mafanikio na changamoto za mfumo mpya wa ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi wa "Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now! - BRN) kwa Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania, Dodoma, tarehe 03 Julai, 2014.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue ameelezea mafanikio na changamoto za Mfumo Mpya wa Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Miradi ya Taifa ujulikanao "Tekeleza  kwa Matokeo Makubwa Sasa" au kwa Kiingereza “Big Results Now! - BRN).

Balozi Sefue alitoa maelezo hayo kupitia mada yake ya “Mafanikio na Changamoto za Mfumo Mpya wa Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Miradi ya Taifa wa "Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa"(BRN) aliyoiwasilisha kwa Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) uliofanyika leo, tarehe 03 Julai, 2014 katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Askofu Stephano R. Moshi, mjini Dodoma.

Kabla ya kuwasilisha mada yake, Balozi Sefue alibainisha kwa wajumbe wa mkutano huo, sababu za Serikali kuamua kutumia BRN ambapo alifafanua kuwa mfumo huu umetokana na tathmini ya kina iliyofanywa  ya utekelezaji isiyoridhisha ya mipango ya maendeleo kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. Balozi Sefue alisema, “ Bila shaka mnakumbuka viashiria muhimu vya Dira yetu hiyo iliyozinduliwa mwaka 2000, ambavyo ni (i) Maisha Bora na Mazuri, (ii) Amani, Utulivu na Umoja wa Kitaifa, (iii) Uongozi Bora na Utawala wa Sheria, (iv) Elimu na (v) Uchumi Imara na Shindani."

Akifafanua zaidi, Balozi Sefue alieleza kuwa Serikali yaTanzania imeamua kuasili mfumo huu kutoka Malaysia, nchi ambayo wakati inapata uhuru wake mwaka 1957, ilikuwa na kiwango cha uchumi sawa na Tanzania Bara ilipopata uhuru wake mwaka 1961. Lakini kwa sasa nchi hiyo inakimbilia kuwa nchi ya kipato cha juu ikiwa na wastani wa pato la kila mwananchi la Dola za Kimarekani 10,687 (2013) kwa mwaka, ikilinganishwa na pato la wastani la dola za kimarekani 742 kwa kila Mtanzania kwa mwaka, kiwango kilichofikiwa mwaka jana (2013).

Utekelezaji wa BRN unafanyika kupitia hatua nane (8) ambazo ni, (i) Kujiwekea Mwelekeo wa Kimkakati, (ii) Kuendesha Maabara Maalum (Labs), (iii) Kuwa na viashiria yakinifu vya kupima matokeo, (iv) Kuweka wazi malengo na vigezo vitakavyotumika kupima utekelezaji, (v) Kufanya kongamano la wazi (Open Day), (vi) Utekelezaji, (vii) Tathmini Huru ya Matokeo ya Utekelezaji na (viii) Kuchapisha Taarifa ya Mwaka.

Balozi Sefue alinukuu kauli ya Mtawa maarufu duniani, Mama Theresa, aliyepata kusema, "Kama huwezi kuwalisha watu 100, jitahidi kufanya hivyo kwa walau mtu mmoja." Akafafanua kuwa kutokana na Serikai nyingi za kiafrika kuwa na changamoto ya kuwa na uwezo mdogo wa kumudu gharama za maendeleo ya watu wake ni busara kuwa na maeneo machache ya vipaumbele, kwa kuanzia. Hii ndiyo maana Serikali iliamua kuchagua maeneo sita (6) ya kipaumbele katika kutekeleza mpango huu kwa kuzingatia mchango wake kwa uboreshaji wa maisha ya wananchi na ukuzaji uchumi ili kuongeza uwezo wa Taifa kukidhi mahitaji yetu.

Maeneo yaliyojumuishwa katika awamu hii ya kwanza ya mfumo huu ni (i) Kilimo, (ii) Elimu, (iii) Nishati ya Umeme, (iv) Maji Vijijini (v) Usafirishaji na (vi) Utafutaji wa Rasilimali Fedha. Maeneo haya yalifanyiwa uchambuzi wa kina na wataalam na wadau mbali mbali  katika Maabara Maalum (Labs) na kuandaliwa programu za utekelezaji. Matokeo ya uchambuzi huo yalitangazwa kwa Umma katika kongamano la wazi lililofanyika tarehe 24 Mei, 2013 katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa mjini Dar es Salaam.

Mafanikio ya mfumo huu yameonekana katika takwimu mbalimbali za kisekta ambazo zilibainishwa kwenye hiyo. Sekta zilizoonyesha mafanikio makubwa  ni Kilimo, Elimu, Nishati, Maji, Usafirishaji, Rasilimalifedha na eneo jipya la Mazingira ya Biashara ambalo maabara yake imekamilika na utekelezaji wake unaanza mwaka huu wa fedha, Julai 2014 - Juni 2015.

Hata hivyo, Balozi Sefue aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo changamoto mbali mbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo huu, ikiwa ni pamoja na changamoto kuu nne (4) ambazo ni:

(i)      Fikra zilizoganda zinazochagiza kufanya mambo kwa mazoea,

(ii)     Mahitaji makubwa ya rasilimalifedha,

(iii)    Urasimu, na

(iv)    Upungufu  wa ujuzi na utaalamu..

Kwa ujumla, Katibu Mkuu Kiongozi alibainisha wazi kuwa Serikali imetiwa moyo sana na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kifupi kupitia BRN.

Katibu Mkuu Kiongozi alihitimisha wasilisho lake kwa kuwashukuru waandaaji na wajumbe wa mkutano huo kwa mwaliko huu mahsusi na pia, kwa kumpa fursa adhimu ya kuwasilisha mada hiyo akaeleza kuwa ana imani kwamba kupitia kwao ujumbe huo utawafikia Watanzania walio wengi kutokana na umuhimu wake.