Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AANZA ZIARA YA KIKAZI KANDA YA ZIWA, JUMATATU TAREHE 4 AGOSTI, 2014


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue ameanza ziara ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa tarehe 4 Agosti, 2014 ambapo ametembelea Mkoa wa Mara. Ziara hiyo inajumuisha Mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza na itamalizika tarehe 6 Agosti, 2014. Katika ziara hii Katibu Mkuu Kiongozi anaambatana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bwana Jumanne Abdallah Sagini, Watendaji Waandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Ikulu.

Ziara hii ni mwendelezo wa ziara za kikazi ambazo  Katibu Mkuu Kiongozi amekuwa akizifanya katika Wizara, Taasisi za Umma, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa kwa madhumuni ya kutoa maelekezo na miongozo mbalimbali, kusikiliza na kujionea hali ya utekelezaji wa majukumu ya Watumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kutolea ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Mara baada ya kuwasili Mkoani Mara, Katibu Mkuu Kiongozi na ujumbe wake walipokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Benedict Ole Kuyan, Viongozi Waandamizi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Wakuu wa Taasisi za Umma na Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali zilizopo Mkoani Mara. Baada ya kusaini kitabu cha wageni, Katibu Mkuu Kiongozi alifanya mazungumzo na Viongozi wa Mkoa ambapo aliwakumbusha umuhimu wa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya Utumishi wa Umma katika kutoa huduma kwa Wananchi.

"Sura ya Serikali kwa Wananchi ipo katika ngazi hii ya Uongozi, hivyo inapaswa na ni muhimu muwasikilize Wananchi matatizo yao, muwahudumie na muwatendee haki wanayostahili", alisisitiza.

Baada ya mazungumzo hayo Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kukutana na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri za Wilaya zilizopo Mkoani Mara, Wakala za Serikali na Taasisi za Umma Mkoani humo. Katika Mkutano huo Katibu Mkuu Kiongozi alitoa fursa kwa Watumishi hao kutoa maoni yao, dukuduku na ushauri kuhusu changamoto mbalimbali za Kiutumishi ambazo zilifuatiwa na ufanunuzi na nyingine kupatiwa ufumbuzi wa hapo hapo.

Katibu Mkuu Kiongozi alihitimisha mazungumzo hayo kwa kusisitiza masuala ya uadilifu, uwajibikaji, uzalendo na bidii katika kutekeleza majukumu yao. Mwishoni mwa ziara yake katika Mkoa wa Mara, Katibu Mkuu Kiongozi alitembelea mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa iliyopo eneo la Kwangwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji mdogo wa Bunda ambayo inatekeleza Mfumo wa Ukusanyaji Mapato Kupitia Dirisha Moja (iTAX), ambapo alipongeza kwa kazi nzuri iliyofanyika na kusisitiza kuwa iwe endelevu ili hatimaye mfumo huo utumike katika halmashauri zote nchini.