Katibu Mkuu Kiongozi atembelea eneo kunakojengwa Mji wa Serikali, Ihumwa Jijini Dodoma leo, tarehe 6-12-2018


Dec 06, 2018

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi, Mhandisi John W. H. Kijazi, leo tarehe 6-12-2018 ametembelea na kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa majemngo ya Ofisi za Serikali katika eneo la Mji wa Serikali lililopo Ihumwa, Jijini Dodoma.

Katika Ziara yake hiyo Katibu Mkuu Kiongozi aliambatana na baadhi ya Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi pamoja na wajumbe wa Kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma. Akiwa katika eneo hilo Katibu Mkuu Kiongozi aliweza kukagua maeneo ya ujenzi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Wakati wa ziara yake hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kuzungumza na wataalam mbalimbali wa Ujenzi pamoja na Watendaji Waandamizi wa Taasisi za serikali ambazo ziko katika operesheni hiyo ya ujenzi, baadhi ya wataalam wa taasisi hizo ikiwemo SUMA JKT, Tanesco, DUWASA, Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), TARURA na Wakala wa Serikali Mtandao, walimweleza Katibu Mkuu Kiongozi hatua mbalimbali walizofikia katika utekelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi.

Akimalizia ziara yake hiyo fupi, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa msisitizo kwa Wataalam hao kutoka taasisi hizo kutekeleza majukumu yao katika mradi huo kwa ufanisi na haraka ili kuweza kufikia lengo la Ofisi za serikali kuhamia katika eneo hilo lilipo Jijini Dodoma.