Katibu Mkuu Kiongozi akabidhi kwa Waziri Mkuu hundi ya zaidi ya bilioni 1 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba, 2016, Mkoani Kagera


Sep 20, 2016

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mha. John W. H. Kijazi, leo tarehe 20 Septemba, 2016 amekabidhi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb), hundi ya shilingi Bilioni Moja, Elfu Thelathini na Mia Moja (1,000,000,030,100/=). Amewasilisha mchango huo kwa niaba ya Watumishi wa Umma kwa ajili ya kuchangia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba, 2016, huko Mkoani Kagera.

Makabidhiano hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makatibu Wakuu, Kaimu Katibu Mkuu, Msajili wa Hazina na Waratibu wa Idara na Vitengo vya Ofisi ya Rais, Ikulu na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi alimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kumpatia nafasi ya kuwasilisha mchango wa Wizara, Idara na Taasisi za Umma kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera.

Katibu Mkuu Kiongozi alisema mchango huo unaenda sambamba na rambirambi za Watumishi wa Umma kwa familia zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika maafa hayo. Aidha, alikiri kuwa mchango uliotolewa hautoshi kurejesha hali ya waathirika wote kama ilivyokuwa kabla ya tetemeko hilo, japo itasaidia kuwafuta machozi na kuwashika mkono ili waweze kusimama tena.

Vilevile, Katibu Mkuu Kiongozi alipongeza jitahada za wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi zenye lengo la kuwasaidia wananchi walioathirika na tetemeko ili waweze kurejea katika hali ya kawaida mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwashukuru Watumishi wa Umma kwa mchango wao ambao alisema umeonesha mshikamano wa dhati katika kuwasaidia wananchi walioathirika na tetemeko hilo. Aidha, aliahidi kufikisha mchango uliotolewa kwa walengwa kupitia kamati za Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mkoa wa Kagera. Waziri Mkuu alimuhakikisha Katibu Mkuu Kiongozi kuwa fedha hizo zitatumika kama zilivyokusudiwa.

Aidha, alijulisha kuwa tathmini ya michango yote iliyotolewa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera itafanyika ili kujua kiasi kilichokusanywa. Kwa msingi huo, aliwakumbusha wote ambao wameahidi na bado hawajawasilisha michango yao kufanya hivyo mapema.

Pamoja na tukio la leo, tarehe 17 Septemba, 2016, Katibu Mkuu Kiongozi alishiriki pia kwenye Matembezi ya Hisani yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ajili ya kuchangisha fedha za kuwasaidia waathirika wa maafa ya tetemeko la ardhi, Mkoani Kagera. Katika tukio hilo, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi alichangia shilingi milioni 3 (3,000,000/=).