Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

ZIARA YA KATIBU MKUU KIONGOZI NA MAKATIBU WAKUU KATIKA MJI WA SERIKALI, MTUMBA - DODOMA


Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka amefanya ziara katika mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma pamoja na Makatibu Wakuu mapema leo, tarehe 5 Oktoba 2023.

Alipokuwa katika ziara maalum ya Makatibu Wakuu ya kutembelea mji wa Serikali Mtumba Dodoma, Mheshimiwa Katibu Mkuu Kiongozi alieleza kuwa mafanikio ya mradi wa ujenzi wa Mji wa Serikali ni kukamilika kwa ukamilifu wake akitolea mfano ujenzi wa Uwanja wa Mashujaa kuwa ni alama kubwa ambao utatumika kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na wageni kujifunza nini ambacho Tanzania imefanya.

“Tunathamini kazi yenu kubwa sana mnayofanya, kama tulivyosema awali kwenye Wasilisho, hii kazi inahitaji Uratibu kwa sababu ni kazi ya Serikali, siyo kazi ya mmoja kuwa amemaliza na wengine kujisikia vibaya, tunashukuru kwa kutupitisha kwenye kazi kuanzia mwanzo, tumeona juhudi kubwa za wataalamu wetu na wasimamizi lakini pia tumeona kazi kubwa iliyopo mbele na tunatambua kwamba baadhi ya wadau wanakaribia kumaliza kazi zao.” Alisema Mhe. Balozi Kusiluka.

Aliendelea kusema kuwa bado kuna muda wa kutosha wa kutatua changamoto ndogo zilizobainika katika ziara hiyo na kusisitiza kuutazama mradi huo kwa ujumla wake kama Serikali moja, na kazi ya uratibu ikiendelea lakini pamoja na kuimarisha timu ya wataalamu wa ngazi zote katika ujenzi na kuwasikiliza, “Ni fursa pekee ambayo tumepewa ya kujenga Makao Makuu ya Serikali mapya na Serikali imetoa fedha nyingi kwa hiyo ni lazima sisi wataalam tufanye kazi inavyopaswa.” Alisisitiza.

Alimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo na kuwapa uhuru wataalam kufanya kazi ya kitaalam inavyopaswa, na kushauri wadau wengi kushiriki katika kazi hiyo pamoja na kujadili mambo ya kitaalam ili watu wengi waweze kujifunza.