Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Mpango wa Maendeleo Uondoe Utegemezi wa Nje: katibu Mkuu Kiongozi


KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ametaka mchakato wa majadiliano ya mpango mpya wa maendeleo utumike kutafuta njia za kuondoa utegemezi katika misaada ya kigeni. Alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam wakati wa kuzindua Mchakato wa Majadiliano ya Kitaifa kuhusu ajenda mpya ya Maendeleo baada ya mwaka 2015 yanayoanza mwezi huu hadi mwanzoni mwa mwaka ujao, lengo likiwa ni kupata maoni ya wananchi ya jinsi ya kusonga mbele.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 50 ambazo maoni ya wananchi yatapelekwa moja kwa moja kwenye ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN), ikiwa ni baada ya kumalizika kwa Mpango wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) inayofikia tamati mwaka 2015. Balozi Sefue alisema majadiliano hayo yaibue njia ya kuondokana na utegemezi na kuongeza uhamasishaji na matumizi ya rasilimali za ndani na kushirikiana na sekta binafsi. “Tunahitaji kufikiria kwa kina cha kufanya baada ya 2015, ili kurithi mfumo wa MDGs ukiwa imara zaidi, wa kujitegemea na kuendeleza kujiimarisha na kujijenga kupitia mafanikio ya MDG,” alisema.

Aliongeza: “Kwa maneno mengine baada ya 2015, ajenda ya maendeleo isichochee utegemezi, lakini ijenge mfumo wa kitaifa, kikanda na kimataifa kukomesha utegemezi, taasisi za kimataifa na washirika wa maendeleo wanatakiwa kuweka mazingira ya kuwezesha kufanikisha hili.”

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Ramadhan Khijjah alisema katika utekelezaji wa MDGs kuna maeneo ambayo Serikali haijafanikiwa hivyo kuhakikisha yanapewa kipaumbele katika majadiliano hayo. Akizungumzia maeneo ambayo nchi haijafanya vizuri, alisema hadi sasa wananchi wengi bado wanaishi chini ya Dola moja ya Marekani na zaidi na kuwataka wananchi kuja na njia ya kukabiliana na tatizo hilo. Pia alisema licha ya kujenga shule na watoto wengi kujiunga, lakini ubora wa elimu, walimu na vitabu vya kiada na ziada ni na matatizo ambayo yanatakiwa kutafutiwa mbinu za kutatua.