Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI Y. SEFUE, AKABIDHIWA KITABU CHAKE CHA KUMBUKUMBU ZA UANACHAMA WA IKULU SACCOS - 03/03/2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, amefurahishwa na uwepo wa vyama vya Ushirika vya Akiba na mikopo (SACCOS) katika taasisi na idara za serikali, na kusisitiza kuwa hilo ni jambo la maana linalotoa fursa kwa watumishi kuwa na kipato cha ziada kitachosaidia kuwaletea ahueni kwani mishahara pekee haikidhi matakwa yao yote.

 Amesema SACCOS ni ​kama ​ benki ya mtu mnyonge, na kusisitiza kwamba mifuko ya aina hiyo inaposimamiwa vizuri faida yake kwa wanachama ni kubwa sana kwani humpa mtumishi ahueni na kumfanya afanye kazi kwa moyo na bila wasiwasi ama msongo wa mawazo.

 Balozi Sefue ameyasema hayo Jumanne Machi 3, 2015 jioni alipokuwa akiongea na Uongozi wa Ushirika wa Akiba na Mikopo wa Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Ikulu, (Ikulu SACCOS), ​uliomtembelea ofisini kwake Ikulu Dar es salaam, kumkabidhi rasmi kitabu chake cha uanachama kufuatia kujiunga kwake na ushirika huo.

 Mishahara yetu ndani ya utumishi wa umma haitoshi kukidhi mahitaji yetu yote, kwa hiyo mipango yote hii ya SACCOS, Mfuko wa Rambirambi na Mfuko wa Ushirika wa Nyumba ​iliyopo hapa Ikulu ​ inafanya maisha ya mtumishi yawe na ahueni sana na kumfanya afanye kazi kwa moyo. Hayo ni mambo ambayo nayaamini sana na nayaunga mkono, na naamini hata Mhe Rais mwenyewe anayaunga mkono na ndio maana amekuwa mwepesi kujiunga na ushirika huu, aliongeza Balozi Sefue.

 Katika hafla hiyo ya makabidhiano, Balozi Sefue alikabidhiwa kitabu namba 2 cha uanachama na Makamu Mwenyekiti wa Ikulu SACCOS Bw. Deodatus Gaudio. Kitabu namba moja cha uanachama wa Ushirika huo amekabidhiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

 Awali, mshauri Mkuu na Mlezi wa Ushirika huo wa Ikulu, Bw. Joseph Sanga, alimfahamisha Katibu Mkuu Kiongozi kwamba mifuko ya SACCOS, Ushirika wa Nyumba na Rambirambi ya watumishi wa Ikulu iko imara na inaendelea kunufaisha wanachama wake kwa ufanisi.

 Bw. Sanga amesema malengo makuu ya mifuko hiyo ni kuleta ustawi kwa watumishi na kwamba wote wanaelewa kuwa mikopo ya SACCOS yao sio kwa ajili ya kununulia chakula ama mavazi bali ni ya kuwekeza kwenye miradi itakayowaongezea kipato.

 Tunataka kwenda mbali zaidi kwa kushirikiana na mfuko wetu ya Ushirika wa Nyumba ambao tayari umepeleka maombi ya ardhi kwa wanachama wake ambapo viwanja vikipatikana tuna mategemeo ya kuwapa mikopo kuvinunua. Mpango huu una faida kwani ni wa amana kubwa na riba ndogo, alisema Bw. Sanga alipokuwa anafafanua kuhusu mipango ya Ikulu SACCOS.