Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi aziagiza Taasisi za Udhibiti kubadilika.


Dar es Salaam 15/05/2023

SERIKALI imezielekeza Taasisi za Udhibiti hapa nchini kubadilika kifikra na kiutendaji ili kuhamasisha na kusaidia maendeleo na ukuaji wa sekta binafsi ambayo bado ni changa na inahitaji ulezi wa serikali.

Rai hii ilitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dr. Moses M. Kusiluka wakati akifungua Kikao cha 43 cha Kamati ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo, 15 Mei 2023. “Wajibu wa taasisi za udhitibiti ni kuwezesha, kuhamasisha na kusaidia ukuaji na ustawi wa sekta binafsi na siyo kuwa kikwazo cha ukuaji wakealisema Dkt. Kusiluka.

Dkt. Kusiluka ameziagiza pia taasisi hizo kwenda sambamba na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuziagiza taasisi hizo kupitia changamoto amnbazo ni kikwazo kwa ukuaji wa sekta binafsi na kupeleka mapendekezo katika Wizara husika ili zifanyiwe kazi.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) amabaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Tendaji ya TNBC, Bi. Angelina Ngalula ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanyia kazi uboreshaji wa mifumo ya utendaji na kuongeza ufanisi kwa baadhi ya taasisi mbalimbali za serikali.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Godwill Wanga amesema, kwa mara ya kwanza sekta binafsi imeipongeza serikali kwa hatua mbalimbali inazozichukua kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Kikao hicho cha Kamati kilikuwa ni maalumu kwa taasisi zote za udhibiti ili kuwa na uelewa pamoja kuhusu ajenda ya Serikali ya kuwezesha na kusaidia ukuaji wa sekta binafsi kwa maendeleo ya Taifa.