Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Teknologia: Mada kuu Mkutano wa Viongozi Dar


TANZANIA imetajwa kuwa nchi pekee Afrika iliyobahatika kutembelewa na marais watatu wa Marekani wakiwa madarakani. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu Majadiliano ya Ushirikiano kwaManufaa ya Wote yanayoanza leo yakihusisha viongozi wapatao 20 kutoka nchi za Afrika . Majadiliano hayo pamoja na masuala mengine, yanahusu matumizi ya teknolojia katika kuhakikisha uzalishaji wenye viwango na ubora.Sefue alisema ujio huo wa viongozi na ziara za marais hao wa Marekani, unatokana na jitihada za Rais Jakaya Kikwete kutembelea nchi hizo na kujenga nazo uhusiano mzuri. Alihakikishia wananchi kutokuwa na wasiwasi katika kufanya shughuli zao za uzalishajimali kwa alichoeleza kwamba ulinzi na usalama ni wa kutosha na Serikali imejiandaa kuhakikisha wageni wanakaa na kuondokanchini salama.

Akifafanua kuhusu majadiliano hayo yanayofanyika Dar es Salaam, alisema viongozi 20 wanatoka Kenya, Uganda, Benin, Algeria, Comoro, Zambia, Togo, Malawi, Burkina Faso, Botswana, Gabon, Lesotho na Malaysia watajadili jinsi nchi inavyoweza kutumia teknolojia kuleta maendeleo ya wananchi kiuchumi na kijamii. Alisema Tanzania ilijiandaa tangu mwaka jana kwa majadiliano hayo katika kanda 11 kwa kushirikisha makundi ya vijana, vyombo vya habari, vyama vya wafanyakazi, afya na makundi mengine kuhusu mbinu za matumizi ya teknolojia kuleta maendeleo kwa njia ya ushirikiano badala ya kila nchi kutafuta peke yake.

Tanzania ilijiandaa tangu mwaka juzi kuwa na mbinu mpya ya kutafuta maendeleo na kupata matokeo ya haraka kwa kutumia teknolojia, kutokana na wazo la Rais Kikwete aliloliibua kwenye mkutano wa mwaka juzi uliofanyika Putrajaya, Malaysia.Tanzania itaongoza majadiliano hayo ya siku nne, ambayo yatashirikisha vikundi vya ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuelimishana na kupeana uzoefu namna ya kutumia teknolojia ili kuleta maendeleo ya haraka. Balozi Sefue alisema kutokana na ujio wa viongozi na wageni wengi nchini, nchi itapata faida kwa kutangaza vivutio vya utalii, biashara na uwekezaji. Balozi alisema, ziara ya Obama ni ya pili kwa Afrika ya kwanza akiwa aliifanya Ghana mwaka 2009.