Wasifu
Mhe. Balozi Hussein A. Kattanga
Katibu Mkuu KiongoziBalozi Hussein A. Kattanga ni Mchumi wa Fedha kwa taaluma. Ana Stashahada ya Juu ya Fedha kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam, Tanzania na Shahada ya Uzamili ya Sayansi (MSc.) ya Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde, Glasgow - Uingereza.
Balozi Hussein A. Kattanga aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 31 Machi 2021, na kuapishwa tarehe 1 Aprili 2021. Katika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi H. A. Kattanga ni Katibu Mkuu wa Rais, Katibu wa Baraza la Mawaziri (BW), na Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa (BUT). Kabla ya uteuzi wake, Balozi H. A. Kattanga alikuwa Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japani, na pia alikuwa akisimamia shughuli za kidiplomasia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na zile za Australia, Papua New Guinea na New Zealand tangu 2020. Kabla ya kuwa na majukumu ya kidiplomasia, Balozi H. A. Kattanga alikuwa Msimamizi na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kutoka Agosti, 2012 hadi Oktoba, 2019.
Balozi Hussein A. Kattanga ana uzoefu wa miaka 27 ya utumishi Serikalini, na kwa zaidi ya miaka 20 amefanya kazi katika nyadhifa za juu Serikalini. Kuanzia mwaka 1986 hadi 2005 alifanya kazi katika Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Mbinga katika ngazi tofauti; Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya-Wilaya ya Mbinga (1996-2005); Mkurugenzi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni - Dar es Salaam (2006-2007); Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) katika mikoa ya Singida na Morogoro (2008-2009); Naibu na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (2010-2011) na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) kuanzia Machi 2011 hadi Agosti, 2012.