Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Wasifu

Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa
Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa
Katibu Mkuu Kiongozi

Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ana Shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma (BA in Political Science and Public Administration); Shahada ya Uzamili (MA); na Shahada ya Uzamivu (PhD), zote kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CKD).  Balozi Dkt. Bashiru alianza Utumishi wa Umma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro kama Mhadhiri Msaidizi kuanzia Septemba, 2003 hadi Septemba, 2004.  Aidha, Balozi Bashiru ametumia taaluma yake kama Mhadhiri (Lecturer) katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma ya CKD kuanzia Oktoba, 2004 hadi Mei, 2018.  Vilevile, amekuwa Kiongozi wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti kati ya mwaka 2014 na mwaka 2016.  Balozi Dkt. Bashiru pia alikuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utandawazi, Mikutano/Mihadhara na Uendelezaji (Director of Internationalisation, Convocation and Advancement) katika CKD. Balozi Bashiru ni mwanafunzi wa falsafa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Baba wa Taifa) kuhusu harakati za ukombozi, sera za kutofungamana na upande wowote, Umoja wa Afrika, ujamaa na kujitegemea.

Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa aliteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa CCM kuanzia Juni, 2018 hadi Februari, 2021.  Uteuzi huo ulitokana na kazi nzuri aliyoifanya akiwa Kiongozi wa Timu iliyofuatilia na kurejesha mali za CCM mwaka 2017/2018.

Tarehe 26 Februari, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alimteua Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi.  Katika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Balozi Bashiru ni Katibu Mkuu wa Rais, Katibu wa Baraza la Mawaziri (BLM), Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa (BUT).