HOTUBA YA MGENI RASMI, MHE. BALOZI OMBENI Y. SEFUE, KATIBU MKUU KIONGOZI, KWENYE HAFLA YA KUMKARIBISHA RASMI MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI, PROF. MUSSA J. ASSAD, HOTELI YA NASHERA, MOROGORO, TAREHE 08 JANUARI, 2015


Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za  Mitaa (LAAC) mliopo hapa,

 

Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu Za Serikali, Prof. Mussa Assad, 

 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro,

 

Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi mliopo hapa

 

Wageni Waalikwa

 

Mabibi na Mabwana

 

Habari za Jioni,

 

            Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, afya njema na kutuwezesha kufikia mwaka mpya wa 2015 na hatimaye kukutanika hapa kwa shughuli hii muhimu. Hivyo, nachukua fursa hii kukutakieni nyote na familia zenu heri na fanaka ya mwaka mpya, 2015.

            Kadhalika, natoa shukrani zangu za kipekee kwa uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa kunikaribisha niwe mgeni wenu katika hafla hii ya kumkaribisha Prof. Mussa J. ASSAD kwenye wadhifa wake mpya wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa kuandaa hafla hii mmefanya jambo jema sana ambalo ni muhimu katika kuimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwenu. Hivyo, naupongeza na kuushukuru uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa uamuzi huu wa busara, ulio sahihi.

Ndugu Watumishi,

            Kama nilivyosema, lengo kuu la hafla hii ni kumkaribisha rasmi Prof. Mussa Juma Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 5 Novemba, 2014. Uteuzi huu umetokana na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Ludovick S.L Utouh, kustaafu kwa heshima kubwa na kwa mujibu wa Sheria mnamo tarehe 19 Septemba, 2014. Kwa hakika Bwana Utouh anastahili pongezi na shukrani tele kwa utumishi wake uliotukuka na uliopandisha sana hadhi ya ofisi hii na kutoa mchango muhimu katika kuimarisha uwajibikaji kwenye matumizi ya Serikali, na Utawala Bora.

 

Nachukua fursa hii kwa namna ya pekee kumkaribisha na kumpongeza sana Prof. Mussa J. Assad, kwa kuteuliwa kushika wadhifa huu mzito wenye dhamana kubwa katika nchi yetu. Kwa sifa, weledi na uwezo alionao, sote tunaamini, kama ambavyo Mheshimiwa Rais anaamini, kwamba atayamudu vema madaraka hayo bila wasiwasi wowote, na kuendeleza kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake.

 

Ndugu Watumishi,

            Najua kuwa ninyi mliopo hapa ni baadhi tu ya watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, na hivyo mnawawakilisha wenzenu wengi waliopo Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Wizarani na Mikoani katika kumkaribisha kiongozi wenu mpya.

 

Ni matumaini yangu kuwa ninyi mliokuwepo hapa mtawawakilisha vyema wenzenu si tu katika kumpokea rasmi kiongozi wenu mpya, bali pia katika kumhakikishia kiongozi wenu kila aina ya msaada na ushirikiano ili aweze kutekeleza vema majukumu yake aliyopewa na Mhe. Rais kwa uwezo, umakini, weledi na uadilifu wake wote. Ni jambo lililo wazi kuwa peke yake Prof. Assad hawezi kufanikiwa; atafanikiwa kwa kadri ya msaada na ushirikiano mtakaompa. Nakuombeni mtoe msaada na ushirikiano huo.

 

Ndugu Watumishi,

Napenda nichukue fursa hii kuwapeni hongera kutokana na kazi zenu za kukagua na kuishauri Serikali. Sisi katika Serikali tumeshuhudia mabadiliko makubwa sana katika utendaji wa kazi wa Ofisi yenu. Licha ya kutoa taarifa za ukaguzi katika muda unaotakiwa, taarifa zenu zimeongeza uwazi na zimeweza kuwafikia wananchi mbalimbali mijini na vijijini. Naamini kuwa kama si weledi wenu, ukichanganywa na usimamizi bora na umakini wa viongozi wenu, tusingefikia hatua tuliyofikia leo. Ninashauri kazi na mafanikio yaliyopatikana yaendelezwe na yadumishwe chini ya kiongozi wenu mpya.

 

Ndugu Watumishi,

Najua kwamba Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ni kazi nyeti na nzito, si hapa Tanzania tu bali pia katika nchi zote zinazozingatia demokrasia, uwajibikaji na uwazi katika kusimamia mapato na matumizi ya rasilimali za umma.

 

Tunajivunia kwamba, Ofisi yenu, kwa kutekeleza dhana ya ukaguzi shirikishi (participatory audit), imeboresha sana uandaaji wa utoaji wa taarifa za mapato na matumizi ya Serikali na kufikia viwango vya kimataifa. Matokeo ya kazi nzuri ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi yameijengea nchi yetu sifa nzuri ndani na nje ya nchi. Ndani ya nchi tumeona maboresho makubwa katika zile Taasisi za Umma zinazofuata ushauri wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na hivyo kupunguza hati zisizoridhisha (adverse opinion) au zenye mashaka (qualified opinion) katika Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wakala za Serikali. Na ninachukua fursa hii kurejea umuhimu wa kila ofisi kuzingatia na kutekeleza ushauri wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hili si jambo la hiari, ni jambo la lazima.

 

Ndugu Watumishi,

            Mimi na wenzangu Serikalini tunatambua mchango wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika maendeleo ya Taifa na kuimarisha utawala bora. Hivyo, mimi binafsi na wenzangu tunaahidi kumpatia ushirikiano wa kutosha, Prof. Mussa J. Assad katika kutekeleza majukumu yake mapya.

 

            Nanyi, watumishi wa Ofisi hii, kama nilivyosema, nakuombeni kila mmoja wenu, na kwa umoja wenu, mumpe ushirikiano kamili ili kwa pamoja mfikie malengo ambayo mmejiwekea. Mshikamano ambao watumishi kwa pamoja mtauonesha miongoni mwenu ni silaha kubwa ya mafanikio na utawezesha Ofisi yenu kuendelea kuimarika na kuaminika ndani ya Serikali na jamii kwa ujumla. Hivyo, chini ya kiongozi wenu mpya ningependa kuona mkiendeleza mafanikio yaliyokwisha kupatikana ikiwemo:

 

  • Kutoa ripoti zenye ufanisi, zilizofikia viwango vya kimataifa, na zinazotolewa kwa wakati.

 

  • Kuendeleza kazi nzuri ya kukagua mahesabu ya Umoja wa Mataifa, hasa kipindi hiki ambacho Tanzania ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa.

 

  • Kuendelea kuimarisha mahusiano ya kiukaguzi kwa kufanya mikutano kabla na baada ya ukaguzi kati ya wakaguzi na wakaguliwa ili kujadili maeneo mbalimbali yatakayokaguliwa wakati wa ukaguzi na athari zake.

 

  • Kuendeleza sifa nzuri ya Ofisi ndani na nje ya nchi.

 

  • Kuimarisha ushirikiano mzuri kati ya Ofisi yenu, Serikali na Bunge. Ofisi yenu imeendelea kuboresha mahusiano mazuri ya kikazi na Mahakama, Serikali na Bunge.  Uhusiano mzuri kati ya vyombo hivi ni muhimu sana kwa ufanisi wa shughuli za Ofisi, lakini bila kuathiri uhuru wenu kikazi. Hili ni muhimu sana maana wakaguzi hawapendwi sana, lakini mtambue wajibu wenu kwa taifa na mfanye kazi zenu kwa haki, uadilifu na weledi wa hali ya juu.

 

  • Mwisho, endeleeni kuweka mkazo kwenye ukaguzi wa thamani (value for money) pamoja na ukaguzi wa matokeo ya matumizi (performance audit). Ninaamini kuwa hili ni eneo muhimu sana kwa kuzingatia ukubwa wa matumizi ya Serikali.

 

Ndugu Watumishi,

            Nashauri kwamba Ofisi hii iendelee kujenga uwezo wa Watumishi wake ili kudumisha sifa na kazi za ukaguzi. Aidha, muendelee kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na weledi mkubwa kwa manufaa na ustawi wa nchi na taifa letu kwa ujumla. Katika kufanya hivyo muendeleze mipango ya elimu na kunoa ujuzi na mbinu za ukaguzi maana wabadhirifu na wezi wa rasilimali za umma nao wanaboresha mbinu zao kila uchao. Lazima wakati wote muwe mbele yao kimbinu.

Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazoikabili Ofisi hii na tunaamini ya kwamba kwa pamoja tunaweza kuzitafutia ufumbuzi.

Ndugu Watumishi,

            Mwisho napenda kukushukuruni nyote mliohudhuria katika hafla hii ya kumkaribisha Prof. Mussa J. Assad kwenye nafasi yake ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Uwepo wenu umefanikisha sana hafla hii.

 

Ndugu Watumishi,

            Baada ya kusema hayo machache napenda kukupongezeni sana tena kwa kuandaa hafla hii na kwa kupata kiongozi mpya. Nami ninayo furaha kumwambia Prof. Mussa J. Assad “Karibu, uchape kazi katika Ofisi hii”

            Nakutakieni usiku mwema, na mafanikio mengi katika shughuli zenu mwaka 2015 na kuendelea.

 

Ahsanteni kwa kunisikiliza