HOTUBA YA KATIBU MKUU KIONGOZI WAKATI WA HAFLA YA KUTOA ZAWADI KWA WAFANYAKAZI BORA/HODARI, KUWAAGA WATUMISHI WALIOSTAAFU PAMOJA NA KUKABIDHIWA VIKOMBE VILIVYOPATIKANA KWENYE MASHINDANO YA SHIMIWI, 2014 IKULU, TAREHE 21 NOVEMBA, 2014.


Katibu Mkuu Ikulu,

 

Mkurugenzi wa Huduma za Ikulu,

 

Wakuu wa Idara na Vitengo,

 

Wafanyakazi Wote Ikulu,

 

Mabibi na Mabwana,

 

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka salama na kutukutanisha leo hii tukiwa na Afya njema. Hili ni jambo la kumshukuru Mungu. Umepita mwaka mzima  tangu tulipokutana kwenye viwanja hivi vya Ikulu. Nadhani muda wote tumeendelea kushirikiana vizuri  kama watumishi wa Ikulu. Nawapongeza wote kwa kujituma katika kutekeleza majukumu mbalimbali yaliyopo mbele yetu.

 

Napenda pia kutumia nafasi hii kuwakaribisha wote kwenye hafla hii fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya mambo matatu muhimu, ambayo ni:

 

(i)                 Kuwapongeza na kutoa zawadi kwa Wafanyakazi Bora/Hodari kwa mwaka 2014;

(ii)              Kuwaaga watumishi waliostaafu kwa mujibu wa Sheria.

 

(iii)            Kupokea vikombe vilivyopatikana katika michezo ya SHIMIWI iliyofanyika mwaka huu na kuwapongeza wanamichezo wote kwa ushindi uliopatikana.

 

Baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi, naomba niseme yafuatayo:

 

Kwanza, kwa niaba ya  Mhe. Rais,  napenda kuwapongeza sana wafanyakazi waliochaguliwa na kupewa heshima kuwa Wafanyakazi Bora na Mfanyakazi Hodari kwa mwaka 2014.   Kuchaguliwa kwenu kunaonyesha jinsi wafanyakazi wenzenu walivyo na imani nanyi. Kuchaguliwa kwenu  uwe ni mfano wa kuigwa na wa kuwahamasisha kuendelea na utendaji bora wa kazi bila kutetereka. Kwa upande mwingine iwe ni chachu ya kuwapa changamoto watumishi wengine waongeze jitihada katika utendaji kazi ili nao mwaka ujao wachaguliwe. Ninawapongeza sana na ahsanteni sana kwa kazi yenu nzuri.

            Pili, nitumie fursa hii kuwapongeza sana wanamichezo wote walioshiriki na kutuwakilisha katika michezo ya SHIMIWI na kupata ushindi mkubwa na hivyo kuiletea heshima Ofisi yetu.

 

Niwapongeze sana kwa kutetea vikombe hivi kwani kwa kufanya hivyo mmeendelea kuzingatia rai yangu ya kuwataka msivipunguze  vikombe bali jitihada zaidi ilenge kuviongeza  mwaka hadi mwaka.

Ndugu Wafanyakazi,

            Natambua kwamba ili timu ishinde, yapo masuala mengi yanayotakiwa kuzingatiwa. Haya ni pamoja na nidhamu, ushirikiano na mazoezi. Sina shaka kwamba Ofisi yetu imewakilishwa na timu ya mfano wa kujituma, nidhamu, ushirikiano na upendo miongoni mwa wanamichezo.      Kushiriki michezo na kufanya mazoezi ya viungo ni muhimu sana kwa kuboresha afya zetu.   Michezo huimarisha nidhamu, uadilifu, moyo wa ushirikiano, ushindani chanya na inaboresha afya ya miili ya wachezaji pamoja na afya ya ubongo.  Kwa hiyo nisisitize kwamba, wafanyakazi wote ni lazima tushiriki kikamilifu  kufanya mazoezi na katika michezo mbalimbali kwa ajili ya kujenga afya zetu.

Nirudie tena yale niliyosema mwaka jana kuwa hata kama muda ni mdogo tafuteni muda wa kufanya mazoezi. Mazoezi mepesi kama vile kutembea mara kwa mara iwe sehemu ya ratiba yenu ya kila siku.

Kwa Wastaafu, ni dhahiri kuwa michezo ni muhimu sana kwa afya zenu, maana kwa umri mliofikia mnakuwa wahanga wa magonjwa ambayo yanaweza kudhibitiwa kwa njia ya kushiriki mazoezi.

 

Wafanyakazi na Wastaafu,

 

Natambua kwamba wenzetu mliostaafu mmeanza ukurasa mpya wa maisha. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kulitumikia Taifa katika nafasi nyingine  kama mlivyofanya mkiwa watumishi wa umma katika ofisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais, Ikulu.

 

Kama sehemu ya kuwaageni, tumewakabidhi Vyeti vya kutambua Utumishi wenu uliotukuka. Hii ni alama tu  na kumbukumbu ya utumishi wenu. Bado inabaki kuwa  changamoto kwetu tuliosalia kuona kama tunaweza kufikia hatua hiyo ya mafanikio mliyopata. Nawapongeza sana kwa hatua mliyofikia ya kustaafu Utumishi wa Umma kwa heshima kubwa. Nasi tukiwa kama Wastaafu watarajiwa tuko mbioni kuwafuata kwani sote ndiko tunakoelekea.

 

Tutaendelea kuwakumbuka kwa yale yote mazuri mliyotuachia na tutayaendeleza, tunawasihi kila inapowezekana msiache kuendelea kutupatia ushauri wenu nasi tupo tayari kuupokea na kuufanyia kazi.

 

 

Ndugu Wafanyakazi,

            Ningependa pia kuchukua nafasi hii kusisitiza masuala machache yanayohusu utekelezaji wa majukumu yetu:

Mosi, ni vema tujenge uelewa wa pamoja wa majukumu tuliyonayo katika Ofisi yetu  na kujenga  ushirikiano wa hali ya juu. Utendaji kazi kwa mazoea lazima ukome sasa. Badala yake kila mmoja wetu kwa nafasi yake afanye kazi kwa malengo yenye kutoa matokeo, ambayo yanapimika na yatapimwa, ili kubaini utendaji kazi wa kila mmoja.  Utendaji wenye kujali matokeo utawezekana endapo sote kwa pamoja tutabadilika kimtazamo na kifikra katika utendaji kazi wetu. Mabadiliko haya ni lazima. Hatuna budi kuhakikisha kwamba wote kwa pamoja tunafanya kazi kwa weledi, kasi zaidi, bidii zaidi kwa lengo la kumwezesha Mheshimiwa Rais kuliongoza Taifa letu kwa ufanisi zaidi tunapoelekea kwenye uchaguzi mwakani.

Pili, tuzingatie Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma wakati wa kutekeleza majukumu yetu ya kila siku na hasa katika matumizi ya fedha za umma. Fedha zilizoidhinishwa hazitoshelezi mahitaji, hivyo sharti zitumike vizuri na kuleta matokeo mazuri yaliyotarajiwa.

Tatu, Tufanye kazi kwa kushirikiana, kuelewana na kwa upendo ili matokeo ya kazi yawe mazuri na endelevu.

Nne, Tuzingatie utunzaji wa siri ili kutoliweka Taifa letu katika hatari.

Tano, Mawasiliano mazuri baina yenu ni nguzo muhimu katika kuleta ufanisi wa kazi. Hivyo, Wakuu wa Idara na Vitengo mnatakiwa kuhakikisha mnaendelea kushirikiana kwa kuwashirikisha watumishi walio chini yenu kwa kuwa na vikao vya mara kwa mara ili kuwawezesha kujua masuala mbalimbali yanayowakwaza watumishi walio chini yenu na kuyatafutia ufumbuzi.

Aidha, kabla ya kumaliza maelezo haya mafupi, nichukue fursa hii kuhimiza umuhimu wa upimaji wa afya zetu ili tuweze kujitambua kama tuna maambukizi ya VVU. Kubainisha kuwa mtu unaishi na VVU kutatusaidia kutambua afya zetu na kuchukua hatua zipasazo kujilinda. Vilevile kutamsaidia Mwajiri kuandaa mipango thabiti ya kuwapatia huduma zote muhimu na stahiki. Aidha, muwe na mazoea ya kupima afya kwa ujumla ili kuzuia magonjwa yanayotibika kabla hayajaleta madhara makubwa.

Mwisho, kwa kuwa tunaelekea mwisho wa mwaka, nitumie  fursa hii ya kukaa pamoja kama watumishi wa Ofisi ya Rais, Ikulu kuwatakia HERI YA KRISMAS NA MWAKA MPYA, 2015.

 

Asanteni sana kwa kunisikiliza.