KATIBU MKUU KIONGOZI AMJULIA HALI WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHESHIMIWA DK. HAMISI KIGWANGALA – AGOSTI 28, 2018


Aug 28, 2018

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mha; John W. H. Kijazi, leo tarehe 28 Agosti, 2018 amemtembelea na kumjulia hali, Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangala, Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye anaendelea kupatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam. Mheshimiwa Kigwangala amelazwa katika Taasisi hiyo kuanzia Agosti 4, 2018 kutokana na majeraha aliyoyapata kufuatia ajali ya gari aliyopata pamoja na wasaidizi wake Agosti 4, 2018 katika Kijiji Magugu, Mkoani Manyara katika barabara kuu ya Arusha - Minjingu – Babati -Dodoma akiwa njiani kuelekea mjini Dodoma kikazi.

Balozi Kijazi alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Lawrence Museru, Mkurugenzi wa Taasisi ya MOI, Dk. Respicious Boniface pamoja na Dk. Samuel L. Swai ambaye ni Mkurugenzi wa Tiba katika Taasisi hiyo. Hii ni mara ya pili kwa Katibu Mkuu Kiongozi kumtembelea na kumjulia hali Mhe. Kigwangala hospitalini hapo, ambapo mnamo tarehe 7 Agosti, 2018 Balozi Kijazi alifanya ziara kama hiyo hospitalini hapo.

Akiwa katika chumba alicholazwa Mhe. Kigwangala ambaye hali yake imeendelea kuimarika kufuatia matibabu anayoyapata, Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kuongea na Mhe. Kigwangala kuhusiana na maendeleo yake na alimtakia kila la heri apone haraka na kuweza kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa Dk. Samuel L. Swai ambaye ni Mkurugenzi wa Tiba katika taasisi hiyo, Mhe. Kigwangala anaweza kuruhusiwa katika siku chache zijazo hii ni kutokana na hali yake kiafya kuimarika, ambapo kwa sasa anafanya mazoezi na kupatiwa muda wa kupumzika na wataendelea kumuangalia kwa muda ili wajiridhishe na hali yake kabla ya kumruhusu, alisisitiza Dk. Swai.

Kwa upande wake Mheshimiwa Dkt. Kigwangala ambaye ni daktari kitaaluma, alimshukuru Katibu Mkuu Kiongozi kwa kuja kumjulia hali na pia aliwashukuru madaktari na wauguzi katika taasisi hiyo ambao kwa kipindi chote alichokuwapo hospitalini hapo wamefanya kazi kwa juhudi na weledi mkubwa ili kuhakikisha kuwa anarudia katika hali yake ya kawaida.

Mwisho Katibu Mkuu Kiongozi aliwashukuru watendaji wote wa Taasisi hiyo kwa utendaji na huduma nzuri wanayotoa kwa wananchi wanaofika hospitalini hapo kupata huduma mbalimbali za afya.