Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

SEKTA BINAFSI YASIFU UTEKELEZAJI WA MKUMBI


Serikali imepongezwa  utekelezaji wa mapendekezo ya sekta binafsi kupitia vikao na mikutano ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ambapo sekta binafsi imekiri kupatikana kwa mafanikio makubwa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) ndani ya  kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Akizungumza mara baada ya kufungua kikao cha 37 cha Kamati Tendaji cha TNBC kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 15 Aprili, 2024, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mheshimiwa Balozi Dkt. Moses Kusiluka amesema sekta binafsi imeridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya sita katika kuboresha na kuweka mazingira na wezeshi ya uwezeshaji na ufanyaji biashara hapa nchini.

 

“Ni faraja kwetu kupata mrejesho chanya kutoka sekta binafsi  kwani inaleta afya sambamba  na kuonyesha dhamira ya kweli kuwa Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuleta mageuzi ya kiuchumi sambamba na kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji,” alisema Balozi Dkt. Kusiluka.

 

Mwenyekiti huyo wa Kamati Tendaji alisema Serikali imeshaondoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa ustawi na ukuaji wa biashara hapa nchini kwa hayo yote ni matunda ya kazi ya Baraza la Taifa la Biashara.

 

Aidha, Balozi Dkt. Kusiluka amelipongeza Baraza kwa kazi nzuri wanayoifanya  ikiwemo kusimamia na kuhakikisha vikundi kazi vyake ambavyo makatibu wakuu ndiyo wenyeviti wa vikundi kazi hivyo.

 

Alisema vikundi kazi vimefanya kazi nzuri ikiwemo kujadiliana na hatimaye kuja na mapendekezo yanayowasilishwa kwenye kikao cha kamati  tendaji kabla ya kupelekwa kwenye mkutano  wa Baraza  mwishoni mwa mwezi Mei au Juni mwanzoni ambapo Mh. Rais ndiye mwenyekiti wake.

 

“Miaka mitatu ya uongozi wa Awamu ya Sita chini ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  imeweza kuboresha na kuimarisha mazingira ya ufanyaji  biashara na uwekezaji  nchini ikiwemo kuchochea ukuaji wa sekta binafsi,” alisema Balozi Dkt. Kusiluka.

 

Naye Mwenyekiti Mwenza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini (TPSF) Bi. Angelina Ngalula ameipongeza serikali kwa kufanya maboresho makubwa na kufanikishwa utekelezaji Mkumbi.

 

 ”Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu zaidi kwa umma na wadau mbalimbali ili waweze kuelewa namna Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) unavyofanya kazi kwani utasaidia kuondoa mkanganyiko baina ya wafanyabiashara na sekta ya umma,” alisisitiza Bi. Ngalula.

 

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt Godwill Wanga alisema kuwa kikao hicho kimeangazia zaidi utekelezaji wa maazimio ya kikao cha 36 cha kamati tendaji ambapo jitihada kubwa zimechukuliwa katika utekelazaji wa maazimio hayo yenye lengo la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

 

Aidha Dkt. Wanga alisema  moja ya ajenda   kubwa iliyojadiliwa ni pamoja na  kuunganisha mifumo ya  Serikali ili weze kusomana   na hivyo kujenga uchumi wa kidijiti utakao chochea na kuongeza tija katika uzalishaji na utoaji huduma  nchini.

 

“Mapinduzi ya  uchumi wa kidijiti  utatoa  mchango mkubwa katika kukuza  pato la mwananchi mmoja mmoja na Taifa kiujumla sambamba na  kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta nyingine za maendeleo na uchumi,” alisema Dkt Wanga.

 

Dkt. Wanga alisema kikao hicho kimeelekeza maswala yote ya udhibiti yahakikishe yanadhibiti zaidi changamoto kuliko kuwadhibiti  wazalishaji ili kutoathiri ukuaji wa uchumi sambamba na    kufanya kazi kwa karibu  na sekta binafsi  ili iweze kuzalisha na kuchangia kikamilifu katika kukuza pato la Taifa.