Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue atembelea Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu na Nyaraka za Serikali, Dodoma, tarehe 30 Juni, 2014


KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI Y. SEFUE ATEMBELEA KITUO CHA TAIFA CHA KUMBUKUMBU, DODOMA, TAREHE 30 JUNI, 2014

 

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue amekitembelea Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu kilichopo Dodoma leo tarehe 30 Juni, 2014,  ambapo amefurahishwa na hatua ya ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo hicho cha aina yake na kikubwa kuliko vyote katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. Katibu Mkuu Kiongozi aliambatana na Maafisa Watendaji Wakuu katika Ofisi ya Rais na alipokelewa na mwenyeji wake  Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bwana George Yambesi, Mkurugenzi wa Idara ya Taifa ya Kumbukumbu na Watendaji wengine Waandamizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

 

Ziara ya Katibu Mkuu Kiongozi Kituoni hapo ni sehemu ya ziara zake za kikazi ambazo amekuwa akizifanya kwenye Wizara, Taasisi za Umma na Idara zinazojitegemea zikilenga pamoja na mambo mengine kuona na kusikia utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwenye sehemu hizo za kazi. Na kwa upande wa Kituo hiki, Katibu Mkuu Kiongozi alikusudia kuona mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizopo tangu Kituo kilipoanzishwa.

 

Akielezea hatua iliyofikiwa hadi sasa, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bwana Yambesi alimwelezea Katibu Mkuu Kiongozi kuwa ujenzi wa Kituo hicho umekamilika na kwamba Kituo kimekabidhiwa rasmi kwa Serikali mnamo tarehe 11 Juni, 2014. Aidha, maandalizi ya ufunguzi rasmi wa Kituo yanaendelea na inatarajiwa ufanywe na Mheshimiwa Rais wakati wowote mwishoni mwa mwezi Julai au mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

 

Katibu Yambesi alielezea baadhi ya  faida zilizopatikana tangu Kituo kilipoanza kazi hadi sasa,ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwezo wa Idara ya Kumbukumbu katika kuhifadhi mafaili 200, 000 hadi 700,000 sawa na maboksi 55,280 hivyo kuokoa nafasi ya mita za mraba 77,700 zilizokuwa zikitumika na Taasisi za Serikali kuhifadhia kumbukumbu, kuleta ufanisi katika utendaji kazi kwa Taasisi za Umma kutokana na kuhamisha na kuteketeza mara kwa mara kwa kumbukumbu zisizohitajika, kupunguza mlundikano wa kumbukumbu katika ofisi mbalimbali za umma,kutumika kikamilifu kwa kumbukumbu zilizohifadhiwa vizuri kituoni hapo, kuokoa kumbukumbu zenye umuhimu wa kudumu kuharibiwa kiholela,kutunza kumbukumbu na nyaraka katika mfumo wa kidigitali hivyo kuwa rahisi kutoa fursa kwa Umma kuweza kuzisoma kwa urahisi na kuwa na Kituo Maridhawa cha kutoa taarifa za Serikali (Trusted National Repistory).

 

Baadhi ya changamoto zilizobainishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi ni pamoja na gharama kubwa ya kukiendesha Kituo hicho dhidi ya ufinyu wa bajeti, ushirikiano kutoka Taasisi za Umma katika kuhamishia kumbukumbu kwenye Kituo hicho na uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za utunzaji wa kumbukumbu katika taasisi za Umma.

 

Baada ya kupitishwa katika sehemu mbalimbali za Kituo hicho, Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kuzungumza na menejimenti na watumishi wa Kituo ambapo alielezea furaha yake kutokana na kazi nzuri iliyofanywa katika kipindi kifupi tangu wazo la kujenga Kituo lilipotolewa hadi sasa. Alirejea kusisitiza kuwa kumbukumbu na nyaraka za taifa ndiyo historia ya nchi na zinapaswa kuhifadhiwa vizuri kwani ndiyo rejea muhimu sana kwa uhai wa taifa.

 

Aliwahimiza watumishi wote katika nafasi zao kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, usiri, weledi na kwa kutumia uwezo wao wakati wote. Akawaasa kuwa Serikali imetumia rasilimali nyingi kujenga mazingira mazuri ya kufanyia kazi hivyo wathamini mazingira hayo ya kazi na wayatunze. Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi aliwahimiza kufuatilia Wizara, Taasisi na Idara zinazojitegemea na kuwahamasisha kuhamishia kumbukumbu zao kituoni hapo kama ilivyokusudiwa.

 

Katibu Mkuu Kiongozi aliuagiza uongozi kufuatilia kwa karibu hoja ya kuipandisha Idara hiyo kuwa Taasisi inayojitegemea na akaahidi kuwa atashirikiana na Watendaji Serikalini kuhakikisha mazingira bora zaidi ya Idara hiyo.