Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI Y. SEFUE, ASHIRIKI AKIWA MGENI RASMI KATIKA MAHAFALI YA TANO YA CHUO KIKUU CHA ST. JOHN TANZANIA NA KUTUNUKU ASTASHAHADA, STASHAHADA NA SHAHADA KWA WAHITIMU, 13 DESEMBA, 2014


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 13 Desemba, 2014 ameshiriki, akiwa Mgeni Rasmi, katika Mahafali ya Tano ya kutunuku astashahada, stashahada na shahada za Chuo Kikuu cha St. John,Tanzania Kampasi ya Dar es Salaam iliyopo Buguruni Malapa.

Katika hotuba yake, Balozi Sefue aliwapongeza wahitimu wa fani mbalimbali kwa kuhimili misukosuko ya masomo hadi kuhitimu, kazi ambayo haikuwa rahisi. "Tunaungana pamoja nanyi katika furaha hii tukiamini suluba ya kitabu na changamoto zake imepita na sasa mnaangalia mbele kwa kujiamini na matarajio mapya", alisema.

Aidha, alieleza kuwa elimu ni silaha kubwa wanayoweza kuitumia kubadili dunia na akawasihi kwa kuanzia waitumie elimu hiyo kujibadili wenyewe, kisha jamii yao na hatimaye nchi yao. Vilevile Balozi Sefue alisisitiza sana suala la uadilifu mahali popote pa kazi watakapoajiriwa iwe serikalini, kwenye taasisi za umma, katika sekta binafsi, ujasiriamali na hata katika kujiajiri wenyewe.

Jumla ya wahitimu mia nne na tisini na tatu (493) walitunukiwa vyeti vyao katika mahafali hayo yaliyofana sana.

 

 

NB: Hotuba kamili ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika tovuti hii sehemu ya hotuba