Habari
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi, Mhandisi John W. H. Kijazi, afanya ziara fupi ya utambulisho Chuo Kikuu cha Dodoma – 29/09/2020
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Mha. John W. H. Kijazi, leo tarehe 29 Septemba, 2020, amefanya ziara fupi ya utambulisho katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Ziara hii fupi ilikuwa mahsusi kwa ajili ya utambulisho kwa uongozi wa baraza pamoja watendaji waandamizi wa chuo hicho.
Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 21 Agosti, 2020, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli, alimteua Balozi, Mha. John W. H. Kijazi kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa chuo hicho, Hayati Benjamin William Mkapa, Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mara baada ya kuwasili chuoni hapo Mkuu huyo mpya wa Chuo Kikuu cha Dodoma alipokelewa na Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Mhe. Gaudentia Kabaka, Makamu Mwenyekiti wa baraza la chuo, Balozi Charles Sanga, Makamu Mkuu wa chuo Profesa Faustin Bee, Naibu Makamu Mkuu wa chuo upande wa mipango, fedha na utawala, Profesa Donald Gregory Mpanduji, Naibu Makamu Mkuu wa chuo upande wa Taaluma, Profesa Alexander Boniface Makulilo pamoja na baadhi ya wakuu wa Ndaki mbalimbali zilizopo chuoni hapo.
Kabla ya kuanza kikao chake na uongozi wa chuo hicho, Balozi Kijazi alipata fursa ya kutumbuizwa kwa ngoma na igizo fupi lililoandaliwa na kikundi cha sanaa za maonyesho kutoka Ndaki ya Sanaa ya chuo hicho, kama ishara ya kumkaribisha mkuu huyo mpya chuoni hapo.
Katika hotuba yake fupi ya ukaribisho, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Baraza la chuo Kikuu cha Dodoma, Mhe. Gaudentia M. Kabaka, alimpongeza Mkuu huyo mpya wa chuo hicho kwa kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli katika ngazi hiyo ya juu katika uongozi wa chuo hicho, na alibainisha wazi imani kubwa aliyokuwa nayo katika utendaji kazi wake ambao utaweza kusaidia katika kutatua changamoto zinazokikabili chuo hicho na kukiwezesha chuo kuwa taasisi bora katika sekta ya elimu ya juu, pia alimtakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yake chuoni hapo.
Akimkaribisha chuoni hapo, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Faustin Bee alitoa historia fupi ya chuo hicho tokea kuanzishwa kwake, uongozi uliotangulia, mafanikio pamoja na changamoto zinazokikabili chuo hicho, ikiwa ni pamoja na uchache wa majengo ya kumbi za mihadhara na ofisi, nyumba za watumishi, usafiri kwa watumishi na wanafunzi, ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo pamoja na tafiti kwa wanafunzi. Pamoja na changamoto hizo Makamu Mkuu wa chuo hicho, aliishukuru serikali hasa kupitia kwa waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Joyce Ndalichako kwa kufanyia kazi changamoto hizo zinazokikabili chuo hicho.
Akitoa neno la shukrani, Mkuu mpya wa chuo hicho, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Mha. John W. H. Kijazi, aliushukuru uongozi wa chuo hicho kwa ukaribisho mzuri alioupata chuoni hapo, “kwa muda mfupi niliokuwa hapa nimefarijika na kujisikia kuwa tayari ni sehemu ya jamii ya chuo hiki, naupongeza uongozi wa chuo pamoja na watumishi wote kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu yenye viwango vya ubora unaokubalika kimataifa pamoja na changamoto zote zinazokikabili” alisema Balozi, Mha. Kijazi. Pia aliwaahidi kutoa ushirikiano mkubwa katika kushughulikia changamoto zote chuoni hapo na aliweka bayana kuwa ataitumia vizuri nafasi yake ya Katibu Mkuu Kiongozi kushughulikia changamoto hizo.
Mwisho aliwashukuru wajumbe wa baraza la chuo hicho kwa kuweza kuwa chombo madhubuti kinachotoa dira ya maendeleo ya chuo hicho mpaka kupiga hatua kubwa katika utoaji elimu ya juu na kufanya tafiti mbalimbali licha ya uchanga wa chuo chenyewe.
Mara baada ya mkutano huo mfupi wa utambulisho, Mkuu huyo wa chuo alipata nafasi ya kutembelea baadhi ya ofisi za utawala ikiwemo ya Makamu Mkuu wa chuo zilizopo katika jengo la utawala chuoni hapo.