Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI ATEMBELEA MKOA WA SIMIYU, JUMANNE TAREHE 5 AGOSTI, 2014


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue amefanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Simiyu tarehe 5 Agosti, 2014. Ziara hii ni sehemu ya ziara yake katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa aliyoianza tarehe 4 Agosti, 2014 ambayo inajumuisha Mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza. Katika ziara hii Katibu Mkuu Kiongozi aliambatana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bwana Jumanne Abdallah Sagini, Watendaji Waandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Ikulu.

Hii ni mojawapo ya ziara za kikazi ambazo  Katibu Mkuu Kiongozi amekuwa akizifanya katika Wizara, Taasisi za Umma, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa kwa madhumuni ya kutoa maelekezo na miongozo mbalimbali, kusikiliza na kujionea hali ya utekelezaji wa majukumu ya Watumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kutolea ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Alipowasili Mkoani Simiyu , Katibu Mkuu Kiongozi na ujumbe wake walipokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa Bibi. Mwamvua Jilusi, Viongozi Waandamizi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Wakuu wa Taasisi za Umma na Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali zilizopo Mkoani humo. Baada ya mapokezi hayo, Katibu Tawala wa Mkoa alimwongoza Katibu Mkuu Kiongozi mpaka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuonana na Mkuu wa Mkoa huo Chifu Paschal Mabiti ambapo alisaini  kitabu cha wageni na kuwa na mazungumzo mafupi na Mkuu wa Mkoa.

Pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu Kiongozi alitembelea wilaya ya Itilima ambayo ni miongoni mwa wilaya mpya zilizoanzishwa kufuatia kuanzishwa kwa Mkoa wa Simiyu. Katika wilaya hiyo Katibu Mkuu Kiongozi alikutana na uongozi wa wilaya ukiongozwa na Mkuu wa wilaya Bibi. Geogina Bundala, na alipata fursa ya kukagua mradi wa ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya wilaya hiyo pamoja na nyumba za watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Baada ya ziara fupi katika wilaya ya Itilima, Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kukutana na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri za Wilaya zilizopo Mkoani Simiyu, Kamati ya Ulinzi ya Mkoa, Wakala za Serikali na Taasisi za Umma Mkoani humo katika ukumbi wa Kanisa la Kilutheri katika Mji mdogo wa Bariadi. Katika Mkutano huo Katibu Mkuu Kiongozi alitoa fursa kwa Watumishi hao kutoa maoni yao, dukuduku na ushauri kuhusu changamoto mbalimbali za Kiutumishi ambazo zilifuatiwa na ufafanuzi na nyingine kupatiwa ufumbuzi wa hapo hapo.

Katibu Mkuu Kiongozi alihitimisha mazungumzo hayo kwa kuwasisitiza watumishi hao kuwa na uadilifu, uwajibikaji, uzalendo na bidii katika kutekeleza majukumu yao, pia aliwapongeza kwa kuwa na moyo wa kujitolea kufanya kazi katika mkoa huo mpya ambao una changamoto nyingi za kiutendaji kutokana na upya wake.

Wakati akihitimisha ziara yake hiyo akiwa njiani kuelekea Mkoani Mwanza, Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kujionea miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea kwa kasi ya kuridhisha katika Mkoa huo mpya.