Habari
Katibu Mkuu Kiongozi akutana na ujumbe kutoka Serikali ya Hungary mjini Dodoma
Katibu Mkuu Kiongozi, leo tarehe 17 Mei, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa watu wanne (4) kutoka Serikali ya Hungary uliokuja Dodoma kwa lengo la kujadili namna Serikali na Sekta Binafsi za Hungary zinavyoweza kushiriki katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini, kupitia uwekezaji, biashara, upatikanaji wa huduma za kifedha na mafunzo.
Ujumbe
wa Hungary uliongozwa na Dkt. Balint Tombor, Mshauri Mkuu wa Kisiasa wa Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, katika masuala ya uchumi na
mikopo aliyeambatana na Mhe. Laszlo Eduard Mathe, Balozi wa Hungary mwenye
makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Dkt. Szues Adam Imre, Mshauri wa Kisiasa
katika Wizara hiyo na Bw. Solomon Kimaro, Konseli wa Heshima wa Hungary nchini
Tanzania.
Kwa
upande wa Tanzania, Makatibu Wakuu wanaosimamia sekta za Uchukuzi, Viwanda,
Biashara na Uwekezaji na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dar Rapid Transit Agency – DART)
walihudhuria.
Katibu
Mkuu Kiongozi aliukaribisha ujumbe huo nchini na kuishukuru Serikali ya Hungary
kwa kuitikia wito wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alioutoa
tarehe 23 Machi, 2017 alipofanya mazungumzo na Balozi Mathe wakati akiwasilisha
hati za kibalozi za utambulishoi, Ikulu, Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo,
Mheshimiwa Rais aliikaribisha Serikali ya Hungary kuunga mkono jitihada za
Serikali ya Tanzania katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza katika
ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha mabasi ya IKARUS hapa nchini.
Aidha,
Katibu Mkuu Kiongozi aliushukuru ujumbe huo kwa kuwasilisha mapendekezo
mbalimbali ya namna Serikali na Sekta Binafsi za Tanzania na Hungary
zinavyoweza kukuza mahusiano ya kiuchumi yenye matokeo chanya kwa pande zote
mbili. Maeneo ya ushirikiano yaliyoainishwa na ujumbe huo ni pamoja na
upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo, misaada ya kiufundi kwa lengo la kujenga uwezo wa wataalam wazawa,
na ufadhili masomo ya Elimu ya Juu kwa Watanzania nchini Hungary.
Kwa
upande wake, Balozi Mathe alielezea dhamira ya Serikali ya Hungary kuhuisha
mahusiano yake ni nchi zinazoendelea, zikiwemo za Kiafrika, ikiwa ni utekelezaji
wa mikakati ya Sera yake mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2014 inayoweka msisitizo
katika kuanzishwa na kuimarishwa kwa mahusiano ya kiuchumi baina ya Hungary na
nchi hizo. “Serikali ya Hungary
imedhamiria kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na nchi za Afrika yenye faida kwa
pande zote” alisisitiza Balozi Mathe.
Serikali za Tanzania na Hungary zimekubaliana kuendelea na majadiliano kwa lengo la kufanikisha azma ya Serikali hizo ya kuimarisha mahusiano ya kiuchumi yenye tija kwa pande zote. Katika kuthibitisha dhamira hiyo, mwezi Julai, 2017 wafanyabiashara kutoka Hungary watafanya ziara nchini kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji na biashara nchini. Serikali ya Tanzania imeahidi kufanya maandalizi stahiki ili kuhakikisha ziara hiyo inafanikiwa.