Habari
Katibu Mkuu Kiongozi, afungua Mkutano wa Faragha wa Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa uliofanyika katika Ukumbi wa Hazina – Dodoma 19 Septemba, 2018.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Mhandisi, John W. H. Kijazi, leo tarehe 19 Septemba, 2018 amefungua mkutano wa faragha wa Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa mikoa uliofanyika katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.
Mkutano huu ambao
umeandaliwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri kwa
kushirikiana na TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu ni muendelezo wa vikao kama
hivyo ambavyo hufanyika kila mwaka kwa kuwakutanisha watendaji hao wa serikali
kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji Serikalini.
Katika hotuba yake ya
ufunguzi Katibu Mkuu Kiongozi aliwapongeza Wajumbe wote ambao wamehudhuria mkutano
huo na hasa wale ambao wamehudhuria kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa katika
nafasi za kiutendaji walizopo. “Hongereni sana kwa kuaminiwa na kupewa
madaraka makubwa ya utendaji katika Serikali hii ya Awamu ya TANO” alisema
Balozi Kijazi.
Aidha, Katibu Mkuu
Kiongozi alisisitiza kuwa mikutano ya aina hii husaidia watendaji wa serikali kufahamiana
vizuri zaidi na kujenga mahusiano mema ya kikazi baina yao, yenye lengo la kuwafanya
kutekeleza kazi zao kama timu moja inayolenga kuwahudumia kikamilifu wananchi
na Watanzania kwa ujumla.
Katika
Mkutano huo, mada mbalimbali zitawasilishwa kwa siku tatu. Mada hizi zinahusiana na kauli mbiu ya
mkutano huo inayosema: Uongozi
makini na wa pamoja unaozingatia uzalendo, uwajibikaji, Utawala Bora na
kusimamia kikamilifu rasilimali za nchi yetu ni nyenzo muhimu kwa watendaji
wakuu wa Serikali kufanikisha lengo la kuifikisha Tanzania kwenye Uchumi wa
Kati. Baadhi ya Mada hizo zina
lengo la kupeana taarifa, na kuelimishana kuhusu taratibu za utendaji kazi
Serikalini, ambapo msisitizo utawekwa katika Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na
Miongozo; Matumizi ya TEHEMA Serikalini; Utawala Bora na Mapambano Dhidi ya
Rushwa; Ulinzi na Usalama; Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya na Majukumu ya
Kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya.
Mwisho
Katibu Mkuu Kiongozi alirudia kuwashukuru tena wajumbe wote kwa kuja kushiriki
katika mkutano huo wa Faragha wa Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Naibu
Makatibu Wakuu wa Mwaka 2018 umefunguliwa rasmi.
NB: Hotuba kamili ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika tovuti yake chiefsecretary.go.tz