Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AFANYA ZIARA MKOANI TANGA - 16 SEPTEMBA, 2014


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, ameendelea na ziara yake ya mikoa ya kaskazini kwa kutembelea mkoa wa Tanga tarehe 16/9/2014. Katika ziara yake mkoani humo, Balozi Sefue alifanya mikutano miwili, katika mkutano wake wa kwanza, alikutana na kuongea na Watendaji Wakuu wa Sekretarieti ya Mkoa na katika mkutano wake wa pili alikutana na baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya mkoa huo na wilaya zake pamoja na watendaji wa Taasisi mbalimbali za Umma zilizopo mkoani Tanga.

Katika mikutano yote miwili Katibu Mkuu Kiongozi aliendelea na utaratibu wake katika kuwakumbusha watumishi wa umma kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma wakati wa kutoa huduma kwa Umma. Katibu Mkuu Kiongopzi alisema kuwa, "Watendaji Wakuu na viongozi wa ngazi mbalimbali hawana budi wakazijua, wakazisimamia na kuzitekeleza sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma. Pia wajenge utamaduni wa kuwaelimisha watumishi walio chini yao ili wazijue na kuzifuata".

Pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuzijua na kuzifuata sheria, kanuni na taratibu hizo, Katibu Mkuu Kiongozi alitahadharisha kuwa, uvujaji wa siri za Serikali usichukuliwe kuwa ni jambo la kawaida. Watumihi wa Umma hawana budi kulipa umuhimu wa pekee jukumu la msingi la kutunza siri za Serikali. Ili kuonyesha umuhimu wa kufanya hivyo, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubw katika utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka zake. Serikali imejenga kituo kikubwa cha kutunza Kumbukumbu na Nyaraka za Serikali mjini Dodoma.

Aidha, ili kurahisisha ubadilishaji taarifa miongoni mwa taasisi za Serikali matumizi salama ya TEHAMA hayana budi kupewa kipaumbele, kwani Serikali kwa kupitia Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) imewekeza na inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya TEHAMA ili kurahisisha mawasiliano salama ndani na miongoni mwa  taasisi zake.

Mwisho Katibu Mkuu Kiongozi, alitoa rai kuwa, Taifa linaelekea katika chaguzi, uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotegemewa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, na uchaguzi wa Serikali Kuu unaotazamiwa kufanyika mwaka 2015. Kuhusiana na chaguzi hizo Katibu Mkuu Kiongozi aliwataka Watumishi wa Umma kutojiingiza kwenye Siasa, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamekiuka masharti ya Utumishi wa Umma, hivyo basi hatua stahiki zitachukuliwa kwa mtumishi yeyote atakayejihusisha na mambo ya kisiasa.

Baada ya kumaliza vikao vyake hivyo Balozi Sefue pamoja na ujumbe wake walipata mapumziko mafupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea mkoani Arusha kuendelea na ziara yake hiyo ambapo tarehe 17/9/2014 atatembelea mkoa wa Manyara na tarehe 18/9/2014 atafanya ziara kama hiyo mkoani Arusha na kumalizia ziara yake hii katika mkoa wa Kilimanjaro tarehe 19/9/2014.