Katibu Mkuu Kiongozi, afungua Mkutano wa Faragha wa Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa uliofanyika katika Ukumbi wa Hazina – Dodoma 19 Septemba, 2018.


Sep 19, 2018

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Mhandisi, John W. H. Kijazi, leo tarehe 19 Septemba, 2018 amefungua mkutano wa faragha wa Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa mikoa uliofanyika katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.

Mkutano huu ambao umeandaliwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri kwa kushirikiana na TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu ni muendelezo wa vikao kama hivyo ambavyo hufanyika kila mwaka kwa kuwakutanisha watendaji hao wa serikali kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji Serikalini.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Katibu Mkuu Kiongozi aliwapongeza Wajumbe wote ambao wamehudhuria mkutano huo na hasa wale ambao wamehudhuria kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa katika nafasi za kiutendaji walizopo. “Hongereni sana kwa kuaminiwa na kupewa madaraka makubwa ya utendaji katika Serikali hii ya Awamu ya TANO” alisema Balozi Kijazi.

Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza kuwa mikutano ya aina hii husaidia watendaji wa serikali kufahamiana vizuri zaidi na kujenga mahusiano mema ya kikazi baina yao, yenye lengo la kuwafanya kutekeleza kazi zao kama timu moja inayolenga kuwahudumia kikamilifu wananchi na Watanzania kwa ujumla.

Katika Mkutano huo, mada mbalimbali zitawasilishwa kwa siku tatu. Mada hizi zinahusiana na kauli mbiu ya mkutano huo inayosema: Uongozi makini na wa pamoja unaozingatia uzalendo, uwajibikaji, Utawala Bora na kusimamia kikamilifu rasilimali za nchi yetu ni nyenzo muhimu kwa watendaji wakuu wa Serikali kufanikisha lengo la kuifikisha Tanzania kwenye Uchumi wa Kati. Baadhi ya Mada hizo zina lengo la kupeana taarifa, na kuelimishana kuhusu taratibu za utendaji kazi Serikalini, ambapo msisitizo utawekwa katika Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo; Matumizi ya TEHEMA Serikalini; Utawala Bora na Mapambano Dhidi ya Rushwa; Ulinzi na Usalama; Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya na Majukumu ya Kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya.

Mwisho Katibu Mkuu Kiongozi alirudia kuwashukuru tena wajumbe wote kwa kuja kushiriki katika mkutano huo wa Faragha wa Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Naibu Makatibu Wakuu wa Mwaka 2018 umefunguliwa rasmi.

NB: Hotuba kamili ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika tovuti yake chiefsecretary.go.tz