Katibu Mkuu Kiongozi akutana na ujumbe kutoka Serikali ya Hungary mjini Dodoma


May 17, 2017

Katibu Mkuu Kiongozi, leo tarehe 17 Mei, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa watu wanne (4) kutoka Serikali ya Hungary uliokuja Dodoma kwa lengo la kujadili namna Serikali na Sekta Binafsi za Hungary zinavyoweza kushiriki katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini, kupitia uwekezaji, biashara, upatikanaji wa huduma za kifedha na mafunzo.

Ujumbe wa Hungary uliongozwa na Dkt. Balint Tombor, Mshauri Mkuu wa Kisiasa wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, katika masuala ya uchumi na mikopo aliyeambatana na Mhe. Laszlo Eduard Mathe, Balozi wa Hungary mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Dkt. Szues Adam Imre, Mshauri wa Kisiasa katika Wizara hiyo na Bw. Solomon Kimaro, Konseli wa Heshima wa Hungary nchini Tanzania.

Kwa upande wa Tanzania, Makatibu Wakuu wanaosimamia sekta za Uchukuzi, Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dar Rapid Transit Agency – DART) walihudhuria.

Katibu Mkuu Kiongozi aliukaribisha ujumbe huo nchini na kuishukuru Serikali ya Hungary kwa kuitikia wito wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alioutoa tarehe 23 Machi, 2017 alipofanya mazungumzo na Balozi Mathe wakati akiwasilisha hati za kibalozi za utambulishoi, Ikulu, Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Rais aliikaribisha Serikali ya Hungary kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha mabasi ya IKARUS hapa nchini.

Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi aliushukuru ujumbe huo kwa kuwasilisha mapendekezo mbalimbali ya namna Serikali na Sekta Binafsi za Tanzania na Hungary zinavyoweza kukuza mahusiano ya kiuchumi yenye matokeo chanya kwa pande zote mbili. Maeneo ya ushirikiano yaliyoainishwa na ujumbe huo ni pamoja na upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, misaada ya kiufundi kwa lengo la kujenga uwezo wa wataalam wazawa, na ufadhili masomo ya Elimu ya Juu kwa Watanzania nchini Hungary.

Kwa upande wake, Balozi Mathe alielezea dhamira ya Serikali ya Hungary kuhuisha mahusiano yake ni nchi zinazoendelea, zikiwemo za Kiafrika, ikiwa ni utekelezaji wa mikakati ya Sera yake mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2014 inayoweka msisitizo katika kuanzishwa na kuimarishwa kwa mahusiano ya kiuchumi baina ya Hungary na nchi hizo. “Serikali ya Hungary imedhamiria kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na nchi za Afrika yenye faida kwa pande zote” alisisitiza Balozi Mathe.

Serikali za Tanzania na Hungary zimekubaliana kuendelea na majadiliano kwa lengo la kufanikisha azma ya Serikali hizo ya kuimarisha mahusiano ya kiuchumi yenye tija kwa pande zote. Katika kuthibitisha dhamira hiyo, mwezi Julai, 2017 wafanyabiashara kutoka Hungary watafanya ziara nchini kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji na biashara nchini. Serikali ya Tanzania imeahidi kufanya maandalizi stahiki ili kuhakikisha ziara hiyo inafanikiwa.